Habari

Sisi ndio marafiki wa kweli, Kalonzo, Wamalwa waambia familia ya Odinga

Na DOMNIC OMBOK December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, na mwenzake wa DAP-K, Eugene Wamalwa, wamejitangaza kuwa marafiki wa kweli wa familia ya Odinga.

Wawili hao jana waliungana na familia hiyo, viongozi na waombolezaji katika mazishi ya Beryl Odinga dada ya aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na seneta wa Siaya Oburu Odinga.

Beryl, mwenye umri wa miaka 72, alizikwa katika shamba la familia ya Odinga eneo la Kang’o ka Jaramogi, ikiwa ni siku arobaini tu baada ya mazishi ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Wamalwa aliwaambia waombolezaji kuwa Muungano wa Upinzani uko imara na unaunga mkono familia ya Odinga.

‘Tunamtakia mema kaka yetu mkubwa Oburu Oginga anayeongoza chama kikubwa cha ODM. Kuna majukumu mengi juu yako,’ alisemwa Wamalwa.

Alihimiza wanachama wa ODM na Dkt Oburu wasisahau marafiki wa zamani ushirikiano mpya wa kisiasa unapozaliwa.

‘Hata ikiwa mtapata marafiki wapya, msisahau marafiki wenu wa zamani. Ikiwa kutatokea jambo na mtahitaji kutafuta marafiki wenu wa dhati, mnaweza kuja kwa Kalonzo Musyoka au Wamalwa,’ aliongeza.

Kiongozi huyo wa DAP-K pia alisisitiza utekelezaji wa ripoti ya NADCO, hususan kuhusu fidia kwa wahanga wa ghasia za baada ya uchaguzi, suala ambalo Raila alikuwa akishinikiza.

Bw Musyoka alisimulia uhusiano wake wa muda mrefu na familia ya Odinga, akielezea kuwa alisoma na Beryl katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

‘Sisi ni wa umri mmoja, alizaliwa mwezi Machi na mimi nilizaliwa mwezi Desemba,’ alisema Kalonzo.

Alieleza kukerwa na ahadi zisizotekelezwa za haki kwa jamii, akisema, ‘Siwezi kukaa kimya ikiwa haki jamii zinakiukwa.’

Seneta Moses Kajwang’ aliuliza ni kwa nini kiongozi mpya wa Waluo anatafutwa wakati familia ya Odinga bado iko.

Alitaja ushindi wa hivi karibuni katika uchaguzi mdogo wa Kasipul, Magarini, na Ugunja kama thibitisho kuwa roho ya Jaramogi na Raila inaendelea kuongoza chama cha ODM.

Kiongozi wa ODM, Oburu Oginga, alikataa wazo lolote la kuwa na pengo la uongozi.

‘Hakuna pengo la uongozi. Raila alituachia viatu vikubwa. Nimepewa viatu hivyo,’ alisisitiza.

Gavana wa Siaya James Orengo alikosoa mwenendo wa siasa wa sasa.

Alilinganisha hali ya sasa na utawala wa Rais Kibaki ambapo watumishi wa umma walizingatia mipaka sahihi.