Makala

Chunga mkwaja usililie chooni, matapeli wa dijitali wameongezeka- DCI

Na BENSON MATHEKA , ERIC MATARA December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Mambo Februari 28 2025, maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) waliwakamata wanaume wawili katika mtaa wa Kileleshwa kwa tuhuma za kumtapeli raia wa China Sh6.5 milioni baada ya kujifanya wataalamu wa ubadilishaji sarafu za kidijitali.

Sarafu za kidijitali ni fedha ya kidijitali inayofanya kazi bila kudhibitiwa na benki kuu au taasisi ya kifedha. Inalindwa na mbinu ya usimbaji fiche na hutumia mtandao usio na udhibiti wa kituo kimoja kupitia teknolojia ya blokcheni.

Wawili hao, waliodai kuwa wataalamu wa sarafu hiyo, walimshawishi raia huyo wa China kuwa wangefanikisha ubadilishaji wa sarafu hiyo, kisha wakatoweka na pesa hizo. Walisakwa na kukamatwa kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kupanga njama ya ulaghai.Wiki mbili zilizopita, wanaume wawili jijini Nairobi pia walipelekwa katika Mahakama ya Milimani kwa tuhuma za kumtapeli mfanyabiashara Sh15.4 milioni katika mpango feki wa uwekezaji wa sarafu ya dijitali.

Walidai wangeweza kumsaidia kufanya biashara kupitia Binance, jukwaa maarufu la ubadilishaji sarafu za kidijitali.Katika kisa kingine mwezi uliopita, wanaume watatu na mwanamke walimtapeli mfanyabiashara mwingine wa Nairobi Sh13.5 milioni kupitia mpango ulioratibiwa kwa ustadi.Katika tukio la hivi majuzi, Novemba 27, maafisa wa DCI walimkamata mshukiwa sugu wa ulaghai huo katika mtaa wa kifahari wa Kiamunyi, Nakuru.

Polisi wanasema mshukiwa huyo, aliyekuwa akitumia majina feki ya Abdirahman Abdikarim na Jamie Damon, alimtapeli mwanamke wa Kilifi Sh3.9 milioni katika mpango tata wa uwekezaji wa kidijitali.

Upelelezi ulianza baada ya mwathiriwa kuripoti kupoteza pesa alizodhani alikuwa akiwekeza katika mfumo halali wa sarafu ya kidijitali.

Polisi walimhusisha mshukiwa huyo na msururu wa ulaghai uliowafanya Wakenya wengi kupoteza fedha katika miaka ya awali.

“Alikuwa ameunda mtandao mpana wa miamala ya kidijitali, majukwaa feki ya uwekezaji wa dijitali na laini za simu zilizosajiliwa kinyume cha sheria, alizotumia kujificha na kuwanasa wawekezaji wasioweza kushuku mpango wake wa utapeli,” alisema Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nakuru, Emmanuel Epuru.

Maafisa wa DCI kutoka Kilifi Kaskazini walifuatilia alama za kidijitali za mshukiwa katika kaunti kadhaa hadi walipompata Nakuru, ambako alikuwa amejificha.Hivi ni miongoni mwa zaidi ya visa 500 vilivyoripotiwa katika miaka mitatu iliyopita, huku DCI ikisema kuna ongezeko kubwa la utapeli wa sarafu za kidijitali unaolenga Wakenya na raia wa kigeni wanaotafuta faida za haraka.

Mwaka 2024 pekee, Wakenya walipoteza zaidi ya Sh5.6 bilioni kutokana na utapeli wa aina hii—ongezeko la asilimia 73 kutoka mwaka uliotangulia, kwa mujibu wa ripoti ya ndani ya DCI.

“Mwaka huu zaidi ya Sh6 bilioni zimepotea. Wapo Wakenya wanaopoteza pesa lakini hawaripoti kwa polisi,” alisema afisa mkuu wa DCI aliyeomba kutotajwa.

Ripoti ya From Risk to Resilience: AI and the Future of Cyber Risk Management, iliyotolewa wiki jana, inaonyesha kuwa Kenya ilipoteza Sh29.9 bilioni kutokana na uhalifu wa mtandaoni mwaka huu, huku Afrika ikipoteza Sh650 bilioni.

Ripoti hiyo imetolewa na Africa Cyber Immersion Centre (ACIC), kitengo cha utafiti cha kampuni ya Serianu Limited, ikishirikisha zaidi ya mashirika 280 yaliyofanyiwa uchunguzi.

Wakati huo huo, Taifa Jumapili imebaini kuwa Wakenya 14 wameorodheshwa na Interpol kwa madai ya kufadhili ugaidi kupitia sarafu za kidijitali na mali nyingine za mtandaoni. Wanne tayari wamekamatwa katika oparesheni ya, Operation Catalyst, iliyofanywa Julai–Septemba 2025 katika nchi sita za Afrika.

Nchini Kenya, wachunguzi walifichua mtandao wa kutakasa fedha kupitia kampuni ya huduma za mali za mtandaoni katika mpango wa Sh55.5 milioni unaoshukiwa kuhusishwa na ufadhili wa ugaidi.

Kwa sababu sarafu kidijitali haina udhibiti wa benki kuu, na miamala yake inategemea mtandao wa kompyuta, matapeli hutumia pengo la ukosefu wa sheria thabiti na kiu ya faida za haraka kuwanasa wawekezaji.Katika ripoti ya Rais William Ruto kuhusu usalama iliyowasilishwa bungeni Novemba 2025, ulaghai wa sarafu za dijitali umetajwa kama tishio kwa usalama wa taifa.

Kutokana na kuongezeka kwa uhalifu huu, DCI imetangaza kuunda kitengo maalum cha kukabiliana na uhalifu wa sarafu za dijitali.

“Tunaunda kitengo maalum kukabiliana na ulaghai wa sarafu za dijitali. Tutaingia katika dijitali ambazo wahalifu hutumia kujificha,” alisema Rosemary Kuraru, Mkurugenzi wa Maabara ya Uchunguzi wa Kisayansi katika DCI.

Kenya ina zaidi ya watu milioni sita wanaomiliki mali za kidijitali, lakini ukuaji huo umewaweka hatarini kutokana na ulaghai, utakasaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi.DCI tayari imeanza mafunzo maalum kwa maafisa wake kuhusu ufuatiliaji wa miamala ya blokcheni, uchunguzi wa pochi za kidijitali na uhalifu unaovuka mipakani. Mafunzo hayo yanadhaminiwa na Umoja wa Ulaya (EU).