Kimataifa

Rais wa Benin asema jaribio la mapinduzi limetibuliwa, aahidi kuadhibu wahusika

Na MASHIRIKA December 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

COTONOU, Benin

RAIS wa Benin Patrice Talon amesema serikali ilifaulu kutibua jaribio la mapinduzi lililotekelezwa na kundi la wanajeshi waasi huku akiapa kuwaadhibu.

Tangazo la Talon alilolitoa Jumapili jioni lilijiri karibu saa 12 baada ya milio ya risasi kusikika katika mitaa kadhaa viungani mwa jiji kuu Cotonou.

Baadaye, wanajeshi waasi walienda katika kituo cha televisheni cha serikali na kutangaza kuwa wamemng’oa mamlakani Talon.

“Lakini wanajeshi wetu watiifu walisimama imara na kukomboa ngome zetu na kuwalemea waasi hao,” akasema kwenye taarifa iliyopeperushwa kupitia runinga za Benin.

Serikali hiyo pia ilipata usaidizi kutoka Nigeria iliyotuma wanajeshi waliopambana na waasi hao.

Rais Talon alisema kutibuliwa kwa jaribio hilo la mapinduzi ya serikali “kulizuia machafuko kushuhudiwa nchini mwetu. Kwa hivyo, waliopanga na kujaribu kutekeleza kosa hilo sharti waadhibiwe.”

Rais Talon aliwapa pole waliojeruhiwa wakati wa jaribio hilo la mapinduzi na wale waliotekwa na wanajeshi hao waasi ambao baadaye walitoroka.

Hata hivyo, shirika la habari la Reuters halikuthibitisha idadi ya waliojeruhiwa kwenye operesheni ya kutibua jaribio hilo la mapinduzi ya serikali nchini Benin.

Jaribio hilo la mapinduzi ni la hivi punde kutokea katika eneo la Afrika Magharibi ambako wanajeshi wametwaa mamlaka katika nchi za Niger, Burkina Faso, Mali, Guinea na mwezi jana nchini Guinea-Bissau.

Lakini hali kama hiyo haikutarajiwa kutokea katika nchi ya Benin ambayo imeshuhudia utulivu kwa miaka 53, tangu mapinduzi ya mwisho kutokea mnamo 1972.

Msemaji mmoja wa serikali Wilfried Leandre Houngbedji alisema kufikia Jumapili jioni watu 14 walikuwa wamekamatwa kuhusiana na jaribio hilo la mapinduzi.