Uncategorized

Tumia likizo ya Desemba kusherehekea ndoa

Na BENSON MATHEKA December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Msimu wa likizo ya Desemba unajulikana kwa sherehe, mapumziko, familia na upendo.

Ni kipindi ambacho ratiba zinapungua, wengi wanapata nafasi ya kupumzika, na moyo wa shukrani unatawala. Ndio maana wataalamu wa mahusiano wanasema huu ndio wakati bora zaidi wa kuchangamkia mapenzi katika ndoa.

Katika warsha moja ya wanandoa iliyofanyika hivi majuzi, mada kuu zilikuwa tatu: kusherehekea mapenzi, kuyadumisha mapenzi na kuchangamkia mapenzi.

Mambo yaliyowasilishwa ni mwongozo muhimu kwa wanandoa wanaotaka kutumia likizo ya Desemba kurejesha cheche na uthabiti wa ndoa zao.

Kwa mujibu wa wataalamu, jambo la kwanza ni kuangalia safari yenu kama wanandoa. Desemba ni wakati mzuri wa kukumbuka mlipotoka, changamoto mlizopitia na ushindi mliovuna. Ni kipindi cha kumpongeza mwenzi wako kwa hatua zake, iwe ni kazi, biashara, imani, au mchango wake katika familia.

“Kuwa pamoja msimu huu kunawapa wanandoa kutambua mafanikio ya kila mmoja na kuimarisha mshikamano wa kiroho na kihisia,” anasema Joseph Mwangi, mtaalamu wa mahusiano ya ndoa.

Mara nyingi wanandoa husahau kuwa mume au mke si mshindani, bali ni mshirika. Kusherehekea mafanikio yake ni kusherehekea yenu wote. Ndio maana wanandoa katika warsha walihimizwa kushukuru wachumba wao na kuwataja kwa maneno mazuri; vitu ambavyo mara nyingi huzidi zawadi yoyote ya kifahari.

“Kipindi hiki cha likizo kinawapa wanandoa fursa ya kujikumbusha furaha yao. Kwa wanandoa waliohudhuria warsha hiyo, wakati wa kucheza uligeuka kuwa njia ya kukumbuka kwamba mapenzi pia yanahitaji ucheshi na msisimko,” asema Mwangi.

Mapumziko ya Desemba pia hutoa nafasi ya kujadili mambo ambayo hayapatiwi muda wakati wa mwaka. Wataalamu wanasisitiza kwamba kimya cha kuadhibu, ni mojawapo ya sumu zinazoua ndoa polepole. Ni muhimu kuzungumza na kukabiliana na migogoro bila kurushiana lawama msimu huu.

“Wanandoa wanapojenga mawasiliano ya heshima na kuzingatia maoni ya kila mmoja, migogoro hupungua na uhusiano hukua kwa amani,” anashauri mtaalamu wa Mahusiano Alice Njeri.

Wanandoa wanahimizwa kuweka mipaka dhidi ya watu wa nje msimu huu wa mapumziko ya Desemba, iwe ni marafiki, ndugu au mitandao ambayo inaweza kuingilia ndoa. Desemba inapaswa kuwa wakati wa kujilinda kama wachumba.

Katika msimu huu pia, wanandoa wanaweza kutambua  “mbweha wadogo” wanaovuruga ndoa: tabia ndogo ndogo kama kutojali, dharau, kupuuza hisia za mwenzako au kutoonyesha upendo na kuzirekebisha.

Msimu huu unafaa kuwa wa kuziondoa na kuanza mwaka mpya kwa amani na ushirikiano.

Desemba ni wakati bora wa kuongeza ladha ya kimahaba katika ndoa. Wataalamu wanashauri wanandoa kutaniana, kupeana muda bora na kujenga ukaribu wa kimwili na kihisia.

“Ukubwa wa furaha ya ndoa unapimwa si kwa zawadi tu, bali kwa muda na mapenzi ya kila siku,” anasema Peter Ochieng, mtaalamu wa tabia za wanandoa.

Anasema huu ni wakati wa kuzungumzia changamoto katika tendo la ndoa. Wanandoa wanaweza kutumia msimu huu kujadili jinsi ya kuboresha shughuli zao faraghani, namna ya kukataa kwa heshima pale mmoja hayuko tayari, na umuhimu wa kupanga muda maalum wa kimapenzi

Mapumziko ya Desemba, asema Ochieng, yanaweza kufanya ndoa kuwa ya furaha. Kwa kusherehekea mapenzi, kudumisha mawasiliano na heshima, wanandoa wanaweza kugeuza likizo hii kuwa mwanzo mpya.