Michezo

Tusker yapiga Sofapaka na kutinga nafasi ya pili KPL

Na CECIL ODONGO December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Tusker jana walipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu (KPL) baada ya kuipiga Sofapaka 2-0 katika uwanja wa MISC Kasarani Annex.

Mabao yote mawili ya Tusker yalifungwa na Ian Simiyu katika kipindi cha pili na sasa wanamvinyo hao wameshinda mechi tatu mfululizo. Simiyu alifunga bao la kwanza kwa kuachilia fataki iliyomlemea kipa wa Sofapaka Edward Olak.

Mvamizi Eric Kapaito aliuwahi mpira na kummegea Dennis Oalo ambaye alimpata Simiyu ndani ya kijisanduka na akafunga bao la pili.

Ushindi huo ulifikisha alama ambazo Tusker imepata hadi 21, sawa na viongozi Kenya Police ambao wana ubora wa mabao.

Hata hivyo, Tusker wamecheza mechi 13 huku Kenya Police wakiwa wamecheza mechi 11 sawa na Gor ambao wapo nambari tatu kwa alama 20.

“Sisi lengo letu lilikuwa kushinda mchuano huo na tumefanya hivyo. Katika kipindi cha kwanza, tulipoteza nafasi kadhaa na nikawaambia wachezaji wangu tujitume kipindi cha pili ndipo tukayapata mabao hayo mawili,” akasema Kocha wa Tusker Charles Okere.

Licha ya kuanza msimu vibaya kiasi kwamba kwa wakati mmoja walikuwa nafasi hatari ya kushushwa ngazi, Tusker sasa imeimarika na Okere anasema wanalenga taji la KPL ambalo wamelishinda mara 13.

Sofapaka nao wapo nafasi hatari ya kushushwa ngazi, wakiwa nambari 17 (nafasi ya pili kutoka nyuma) kwa alama 12 baada ya mechi 13.