Kimataifa

Congo yasema M23 bado wako Uvira licha ya kudai kujiondoa

Na MASHIRIKA, WINNIE ONYANDO December 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kuwa waasi wa M23 bado hawajajiondoa kwenye mji wa Uvira ulioko Kivu Kusini kama walivyotangaza Desemba 16, 2025.

Licha ya tangazo hilo, waasi wa M23, bado wako Uvira, mashariki mwa Congo, na mapigano yanaendelea katika maeneo ya karibu.

Kulingana na vyanzo rasmi, licha ya tangazo la kundi hilo la waasi wa M23, wapiganaji wenye silaha bado wanaonekana katika mji huo.

Waziri wa Habari na Msemaji wa Serikali, Patrick Muyaya amewashutumu waasi hao kwa kuendeleza vita, siku chache tu baada ya kusaini makubaliano ya amani.

“’Huu ni upotoshaji. Inakuwaje shinikizo limewekwa wazi kwa Rwanda, sasa M23 ndio inajitokeza ikisema, “tumekosa na tunaondoka Uvira”?  Ni dhahiri huu ni ujanja wa kumvuruga mpatanishi ambaye ni Amerika iliypjitolea kuchukua hatua, kwa sababu ni wazi kuwa kilichotokea Uvira hakikubaliki.”

Hata hivyo, mapigano yanaendelea kusini mwa mji wa Uvira katika eneo la Makobola na milima ya Swima na Kasekezi katika tarafa ya Fizi, kati ya jeshi la Kongo, FARDC, wakishirikiana na Wazalendo dhidi ya waasi wa M23 wanaotaka kusonga mbele kuelekea mji wa Baraka.

Hali hiyo inazusha hofu katika jamii na kusababisha maelfu ya familia kukimbia makazi yao jambo ambalo Waziri Muyaya amekiri akisema, “Leo, tuna takwimu ya wakimbizi 200,000. Hali ni tete. Ni wazi, tutafanya kilatuwezalo, kuhakikisha kwamba tunatoa makazi, na kuhakikisha wenzetu wanatunzwa vyema popote walipo.”