Makala

Hizi ndizo sababu za kidini za kumzika Muislamu haraka

Na CECIL ODONGO December 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kwa jina la Mwenyezi Mungu wa kuneemesha neema ndogondogo na neema kubwa kubwa tumejaaliwa kukutana kwenye ukumbi huu ambapo leo maada yetu ni kuhusu kifo na mazishi ya muumini wa Kiislamu.

Maswali yameibuka kwa nini Waislamu kuzikwa haraka kutokana na mauti ya Jaji wa Mahakama ya Juu Mohamed Ibrahim na mwanasiasa na waziri wa zamani Cyrus Jirongo.

Jaji Ibrahim alizikwa jana katika makaburi ya Kariakor Nairobi kwenye hafla ambayo ilihudhuriwa na wakuu wa mahakama na viongozi wa kidini. Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un na sote tunapitia njia hiyo hiyo ya nafsi yetu kuonja mauti.

Swali hata hivyo ni kwa nini Muislamu anazikwa haraka au ndani ya saa 48?

Kwa mujibu wa Mkuu wa Daawah kwenye Msikiti wa Jamia Sheikh Mohamed Sheikh, Mtume Mohamed (S.A.W) anasema kuwa mtu akifa lazima azikwe haraka iwezekanavyo.

“Mtume anasema akifa, anaambia Ummah (Waislamu wanaoishi), ‘fanya haraka na unizike’.”

Kwa mujibu wa Sheikh Mohamed, mazishi ya Muislamu huwa yanastahili kufanyika haraka na familia inapewa siku tatu za kuomboleza baada ya mazishi.

“Msingi wa kuzika haraka ni kuepushia familia siku kadhaa za dhiki na pia kuhakikisha kuwa gharama ile ya mazishi inapungua. Mali ya marehemu inastahili kuwafaa wale ambao wamesalia badala ya kutumika kwenye matanga na shughuli zinazotokea,” akaongeza Sheikh Mohamed.

Ndani ya huo muda wa saa 48 baada ya kufariki, maiti ya Muislamu huoshwa na jamii yake na marafiki kisha hufungwa vizuri kisha kuswaliwa msikitini kabla ya kuzikwa.

“Muislamu huzikwa kama kichwa kinaangalia Mecca jinsi alivyofanyiwa mtume. Aidha ni vyema azikwe kwenye makaburi ili familia yake iweze kutembelea kaburu lake na kumwombea dua,” akasema.

“Pia kumzika Muislamu nyumbani huwa si nafuu kwa sababu akizikwa kule nyumbani, familia yake huandamwa na msongo wa mawazo kwa kipindi kirefu kutokana na kuliona kaburi lile,” akasema.

Msomi huyo wa dini anasema kuwa Muislamu anaweza kuzikwa mahala popote alipofia kwa sababu Allah anaamini ardhi yote iko sawa na inaweza kumsitiri muumini wake wakati wowote.