• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Christine Kathure Kendi: Haijalishi umetoka wapi

Christine Kathure Kendi: Haijalishi umetoka wapi

Na JOHN KIMWERE

‘MTAKA cha mvunguni sharti ainame”. Hivi ndivyo wahenga walilonga tangu azali. Ni msemo ambao umeonekana kuwa na mashiko kwa kiwango fulani miongoni mwa jamii.

Pia msemo huo unaonekana unaendelea kudhihirishwa na kina dada wengi tu ambao wamejitolea mhanga kujituma kwenye masuala tofauti kusaka riziki.

Miongoni mwao ni mwadada Christine Kathure Kendi anayekiri kwamba amepitia pandashuka nyingi tu hasa kuanzia utotoni mwake. Binti huyu ni kati ya waigizaji wanaokuja anayejiamini ana uwezo tosha kutinga levo ya kimataifa miaka ijayo.

”Hakika napenda kuigiza na ndiyo maana ninaamini ipo siku nitafanikiwa kushiriki muvi zitakazopata mpenyo na kupeperushwa kupitia stesheni ya Maisha Magic East,” alisema Kendi kwenye mahojiano na kuongeza kwamba waigizaji wanaoibukia nyakati zote wanastahili kutumia muda wao vizuri na kuelewa kwamba wanajijengea maisha ya baadaye. Kathure ni mshirika wa kundi la U-Tena lililobuniwa zaidi ya miaka kumi chini ya mwavuli wa Shirika la Hope World Wide la mtaani Mukuru Kwa Reuben.

Katika kundi hilo alibahatika kushiriki shoo za michezo ya kuigiza ‘Jipange Festivals’  waliyoitumia kuhamasisha jamii kuhusu ugonjwa wa Ukimwi.

Kupitia shoo hizo alibahatika kutwaa tuzo ya ‘Best Actress’ pia ‘Best Play’.

Anasema ana imani tosha atapata nafasi ya uigizaji karibuni maana ameketi mkao wa subira anakotarajia nafasi za kushiriki majaribio ya uigizaji.

”Nimekawia bila kushiriki muvi yoyote lakini ninaamini nipo darasani ninakojifunza mambo tofauti,” alisema na kuongeza kwamba ni jambo la kawaida katika taaluma ya uigizaji.

Mwanadada huyu anajivunia kuanzisha kundi la ‘No Young Single Parenting’ analosema ndilo sauti ya wanadada ambao hawajaolewa, waliopata watoto nje ya ndoa ‘The Voice of Single Mums’ ambalo wanachama wake ni wakazi wa Mtaa wa
Mukuru Kwa Njenga.

Christine Kathure Kendi. Picha/ John Kimwere

Anasema kupitia mradi huo nalenga kufundisha wana dada sampuli yangu waliopata watoto nje ya ndoa kuwa wabunifu ili kupata namna wanavyoweza kujitafutia riziki baada ya pengine kuachwa kwa mataa na baba za wana wao.

Kisura huyu huyu anajivunia kushiriki filamu za TV-Series zilizopeperushwa kupitia KTN kipindi cha ‘Gavana’ mwaka 2014 hadi 2015. Aidha aliwahi kuigiza kipindi kilichokuwa maarufu nchini miaka iliyopita cha ‘Vitimbi’ kilichokuwa kinaonyeshwa kupitia runinga ya KBC.  Pia alikuwa miongoni mwa waigizaji katika kipindi cha vichekesho cha redio ‘Jongo Lover’ pia ‘Well Told Stories’ (WTS) kilichokuwa kinarushwa Ghetto FM. Vilevile alikuwa kati ya wazalishaji wa kipindi cha televisheni cha
KU-Mashinani mwaka 2015.

Anasema akishirikiana na wenzake waliokuwa washiriki kipindi cha ‘Gavana’ wameanzisha brandi yao Artisque Productions wanakolenga kufanya projekti zao na kuzitafutia soko katika mojawapo kati ya runinga za humu nchini.

Anakiri kwamba uigizaji ulimuokoa pakubwa alipokosa karo ya kumwezesha kuendelea na elimu ya sekondari ambapo  pengine angejikuta akijiunga na makundi ya uhalifu mitaani.

”Ninasema hivyo kwa kuzingatia maisha katika mitaa ya mabanda hufanya vijana wengi kujiunga na makundi ya uhalifu kwenye juhudi za kujitafutia riziki,” alisema.

Kadhalika anatoa mwito kwa wanadada wenye talanta ya uigizaji kujiwekea maono na kumtumaimia Mungu nyakati zote.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Tathmini ya kina kuhusu dhana ya...

Helb yafafanua alichomaanisha Waziri Amina Mohamed

adminleo