Utahama vyama mpaka uvimalize ila Kilifi 2027 bado ni Mung’aro, ODM wamwambia Jumwa
VIONGOZI wa Chama cha ODM katika Kaunti ya Kilifi, wamepuuzilia mbali hatua ya aliyekuwa waziri wa jinsia, Bi Aisha Jumwa, kujiunga na Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) ili kuwania ugavana 2027.
Bi Jumwa alitumia Chama cha UDA mwaka wa 2022 kuwania wadhifa huo akashindwa na Bw Gideon Mung’aro wa ODM, lakini akahamia PAA kinachoongozwa na Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi, hivi majuzi.
Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi, alisema Bw Mung’aro ndiye kigogo wa siasa za Kaunti ya Kilifi kwa hivyo wakazi wamuunge mkono.
“Katika masuala ya kisiasa hapa Kilifi lazima tushirikiane na Gavana wetu Bw Mung’aro ambaye ndiye msemaji wetu wa kisiasa,” alisema Bi Mnyazi.
Mbunge huyo pia alimpigia debe Rais William Ruto kwa kuteua mawaziri wawili ambao ni Bw Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Baharini) na Bw Salim Mvurya (Michezo) pamoja na makatibu watano kutoka Pwani.
“Lazima turudishe mkono kwa Rais Ruto. Tulinyakua ushindi wa kiti cha ubunge wa Magarini sababu ya ushirikiano na serikali,” alisema Bi Mnyazi.
Mbunge wa Kaloleni, Bw Paul Katana, alisema viongozi wa Kilifi wataendelea kushirikiana na Bw Mung’aro kisiasa na maendeleo.
Aliwataka wakazi kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza bila kuyumba.
“Marehemu kinara wetu wa ODM, Bw Raila Odinga alituacha serikalini na tutasalia humo. Mwenyekiti wa chama cha ODM Kilifi ni Bw Mung’aro. Tukitaka maendeleo tusalie serikalini,” alisema.
Aliwaonya wakazi dhidi ya kumsaliti Gavana Mung’aro ifikapo Uchaguzi Mkuu wa 2027.
“Wakati wa siasa haujafika, watakuja hivi karibuni na kuwapa madera ya samawati, zichukueni hata pesa chukueni mkale. Lakini msisahau mahali ambapo mpo muende mujiingize kwenye shida,” alisema Bw Chonga.
Katibu wa Vijana na Michezo Fikirini Jacobs, aliwaonya wakazi dhidi ya kushabikia siasa za upinzani.
“Ninawaonya wazazi wangu, msiwasikize hao. Sisi tuko ndani ya serikali na tunamuunga mkono Rais Ruto kwa faida za serikalini. Kama si hii serikali singekuwa katibu,” akasema.