Wanga: ODM haitakuwa upinzani tena 2027
ODM imetangaza misururu ya shughuli za mashinani kama njia ya kujipanga na kuweka mikakati ya kura ya 2027.
Gavana wa Homa Bay, Gladys Wanga ambaye pia ni mwenyekiti wa chama amesema kuwa lengo lao ni kujivumisha zaidi ili watwae mamlaka kwenye uchaguzi huo.
Bi Wanga alifafanua kuwa wanalenga kuunda serikali kama chama au kwa kuingia katika muungano ambao wana uhakika utawapa ushindi.
“Tunaendelea kujivumisha na kuhakikisha tupo imara nyanjani kwa maandalizi ya 2027. Katika uchaguzi huo tunalenga kutwaa mamlaka kama muungano au chama huru na uhusiano wetu wa sasa na Kenya Kwanza upo tu hadi 2027,” akasema Bi Wanga.
Kumekuwa na madai kuwa chama hicho ndicho huzembea na kukosa kumakinika kisha baadaye huja kulalamikia wafuasi wake kuwa imechezewa shere kwenye uchaguzi.
“Ukiangalia hata 2017 tulishinda na tukachezewa shere lakini Mahakama ya Juu ikafuta matokeo yaliyotangazwa. Ukitaka kufahamu tumekuwa tukishinda uchaguzi, angalia idadi ya madiwani, magavana na hata washikilizi wa nyadhifa nyingine,” akasema Bi Wanga.
Wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya ODM jijini Mombasa, uongozi wa ODM ulitangaza kuwa mara hii lazima wahakikishe wapo mrengo ambao unapata ushindi kwa sababu wamechoka kuwa katika upinzani.
Gavana huyo sasa anasema ODM lazima iwe serikalini katika kura ya 2027 huku akikumbuka jinsi mambo yamewawia magumu katika chaguzi nne zilizopita alizodai wamekuwa wakipata ushindi.
Alitaja wizi wa kura katika uchaguzi wa 2007 aliousema umevumiliwa na chama cha chungwa tangu kibuniwe mnamo 2005.
Aidha gavana huyo alisema chama kimekuwa kikiathirika na propaganda kwa sababu wapinzani wake wamekuwa wakikisawiri na kukihusisha na siasa za fujo.
Hii ni licha ya kuwa wao wamekuwa wakipigania mabadiliko ya kisheria kuhakikisha uwazi kwenye uchaguzi.
“ODM imekuwa barabarani ikipigania mabadiliko na wale ambao huleta shida ni maafisa wa usalama. Tumechangia sana kupanuliwa kwa demokrasia na iwapo hilo ndilo linaitwa ghasia, basi iwe hivyo,” akasema.
“Hata hivyo tumeimarika kutokana na jinsi tunavyoongoza shughuli zetu na si vyema kutuhusisha na ghasia tena,”
Kati ya visa ambavyo vinafanya ODM irejelewe kama chama cha ghasia ni fujo ambazo zilishuhudiwa wakati wa kuwachagua maafisa wapya wa chama mnamo 2014 uwanjani Kasarani
ODM imekuwa ikikumbwa na mgawanyiko mkubwa tangu mauti ya Raila mnamo Oktoba 16.
Tangu 2005 ODM imekuwa dhabiti chini ya uongozi wa marehemu Bw Odinga ambaye maamuzi yake ya kisiasa yamekuwa kama sheria kwa wafuasi wake.
Hata hivyo tangu mauti yake, kuna mirengo ambayo imekuwa ikipinga kuendelea kwa ushirikiano na Rais William Ruto, mwingine ukiunga na mwingine ukitaka Kongamano la Kitaifa la Chama (NDC) ili kumteua atakayekuwa akishauriana na rais masuala ya Serikali Jumuishi.
Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga na kundi la viongozi wa mrengo wake hata hivyo wamekuwa wakisisitiza kuwa chama kiko serikalini hadi 2027 na kitafanya uamuzi wa kuendelea au kujiondoa uchaguzi huo ukikaribia.
Mawaziri John Mbadi (Fedha) na Opiyo Wandayi (Kawi) nao wamekuwa wakisema kwamba watamuunga mkono Rais 2027 wakisema hakuna kiongozi yeyote ndani ODM anayetosha viatu vya Raila.
Bi Wanga anasema ufanisi mkubwa wa chama hicho ni kupigania Katiba ya 2010 ambayo ilileta mfumo wa ugatuzi.