Dimba

Timothy Ouma wa Harambee Stars arudisha mkono

Na TOTO AREGE December 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KATIKA ishara ya kusherehekea na jamii wakati huu wa kukaribisha krimasi,

Timothy Ouma wa Harambee Stars arudisha mkono

Jumatatu, alisherehekea na vijana kutoka mtaa wa Kawangware katika Shule ya Msingi ya Dagoretti Muslim Kawangware, Nairobi alikokulia.

Ouma, anayeipigia klabu ya Lech Poznań ya Poland, alikutana na familia mbalimbali kutoka mtaa huo pamoja na wachezaji chipukizi.

Hafla hiyo ililenga kuinua jamii kwa kutoa chakula kwa familia kama sherehe ya mapema ya Krismasi na kusambaza mipira ya soka na jezi kwa timu za vijana.

“Nililelewa katika jamii hii (Kawangware) na niko hapa nilipo leo kwa sababu ya watu hawa. Wamechangia ukuaji wangu kwa njia moja au nyingine. Nimecheza katika karibu kila uwanja wa soka karibu na Kawangware na Dagoretti na ninarejesha mkono  ili kuonyesha kuwa kuna matumaini hasa kwa kizazi kipya.”

“Kutoka katika mazingira haya duni, ninaelewa vizuri jinsi familia zinavyohangaika kuweka chakula mezani. Sio wote wana bahati ya kuwa na sherehe za Krismasi. Inaweza kuwa si kubwa au ya kutosha lakini hakika inaweza kuleta tabasamu kwa watoto na kinamama katika kipindi hiki,” alisema Ouma.

Wachezaji wengine wa Stars waliohudhuria ni pamoja na beki Rooney Onyango wa klabu ya Norway ya Sogndal Football, na mlinda lango wa Gor Mahia Byrne Omondi.