Kimataifa

Ukraine haina haraka ya amani, asema Putin akiendelea kuinyeshea makombora

December 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MOSCOW URUSI

RAIS Vladimir Putin amesema Ukraine haina haraka ya amani na ikiwa haitaki kusuluhisha mgogoro wao kwa njia ya amani, Moscow itafanikisha malengo yake kimabavu.

Matamshi ya Putin mnamo Jumamosi yaliyopeperushwa na idhaa ya taifa ya TASS, yalitokea baada ya mashambulizi makali ya droni na makombora yaliyotekelezwa na Urusi na kusababisha Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, kusema Urusi inadhihirisha nia ya kuendeleza vita huku Kyiv ikitaka amani.

Zelenskiy alitazamiwa kukutana na Rais wa Amerika, Donald Trump, jijini Florida jana kutafuta suluhisho la vita vilivyoanzishwa na Putin karibu miaka minne iliyopita kwa kuvamia jirani yake ‘mdogo’.

Ikulu ya White House haikujibu mara moja ombi la kupata kauli ya Putin.

Makamanda wa Urusi walimweleza Putin wakati wa ziara ya ukaguzi kwamba Moscow iliteka miji ya Myrnohrad, Rodynske na Artemivka iliyopo eneo la Ukraine Mashariki ikiwemo Huliaipole na Stepnohirsk katika eneo la Zaporizhzhia, Kremlin ilisema kupitia mtandao wa Telegramu.

Jeshi la Ukraine lilikanusha madai ya Urusi kuhusu Huliaipole na Myrnohrad likisema kuwa ni taarifa za uongo.

Zelenskiy na Trump walipangiwa kukutana jana kupanga mikakati ya kuzima vita Ukraine, lakini wanakabiliwa na tofauti kubwa kuhusu masuala muhimu na uchokozi kupitia mashambulizi ya angani ya Urusi.

Urusi iliishambulia Kyiv na maeneo mengine ya Ukraine yanayokumbwa na mapigano huku mamia ya makombora na droni Jumamosi zikizima umeme na mifumo ya joto katika sehemu za jiji kuu.

Zelenskiy alitaja mashambulizi hayo kuwa jibu kwa juhudi zinazoendelezwa na Amerika kufanikisha amani.

Zelenskiy alieleza wanahabari kuwa alikusudia kujadili hatima ya eneo la Ukraine la Donhas linalogombaniwa katika kikao kwenye makazi ya Trump, Florida, pamoja na hatima ya kiwanda cha nishati ya nuklia cha Zaporizhzhia, miongoni mwa masuala mengine.

Rais wa Ukraine na wajumbe wake waliwasili Florida mnamo Jumamosi, naibu waziri wa Masuala ya Kigeni Ukraine, Serhiy Kyslytsya, alisema kupitia X.

“Masalkheri, Florida!” aliandika Kyslytsya, akiambatisha ujumbe huo na picha ya ndege iliyobeba jina la rais wa Amerika.

Moscow imesisitiza mara kwa mara kwamba Ukraine isalimishe Donbas, yote hata maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Kyiv, na maafisa wa Urusi wamepinga vikali sehemu nyingine za pendekezo jipya, na kuibua shaka kuhusu iwapo Rais Putin atakubali chochote kitakachotokana na mazungumzo ya jana.

Huku Moscow ikisisitiza kupata Donbas yote, Kyiv inataka ramani hiyo isimamishwe kwenye mikondo ya sasa ya mapigano.

Amerika, ikitafuta suluhu, imependekeza eneo la biashara huru ikiwa Ukraine itaondoka eneo hilo, ingawa bado haijabainika ni vipi eneo hilo litaendeshwa kihalisia.

Zelenskiy, ambaye mikutano yake ya awali na Trump haijawa ikienda vyema kila mara, anahofia pamoja na wandani wake wa Uropa kwamba Trump huenda akauza Ukraine na kuacha mataifa makuu ya Uropa yakigharimia kwa kuunga mkono taifa lililozoroteshwa, baada ya vikosi vya Urusi kuteka kilomita 12 hadi 17 mraba (maili 4.6-6.6 mraba) za eneo lake mnamo 2025.

Urusi inadhibiti Crimea yote, iliyotwaa 2014, na tangu ivamie Ukraine karibu miaka minne iliyopita, imedhibiti takriban asilimia 12 ya eneo lake ikiwemo karibu asilimia 90 za Donbas, asilimia 75 za maeneo ya Zaporizhzhia na Kherson na vijisehemu vya Kharkiv, Sumy, Mykolaiv na Dnipropetrovsk, kulingana na makadirio ya Urusi.