Kimataifa

Polisi waendelea kumzuilia mkosoaji mkuu wa Museveni Sarah Bireete uchaguzi ukikaribia

January 2nd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

POLISI nchini Uganda wanaendelea kumzuilia mwanaharakati maarufu huku utawala wa Rais Yoweri Museveni ukiendelea kuwaandama wapinzani na wakosoaji kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 15, 2026.

Polisi walithibitisha kuwa Sarah Bireete ambaye ni mwanaharakati na mkosoaji mkubwa wa serikali hasa nyakati za mahojiano kwenye runinga mbalimbali za Uganda, anaendelea kuzuiliwa.

“Anaendelea kuzuiliwa na polisi na atafikishwa mahakamani wakati wowote,” ikasema taarifa ya polisi bila kufichua siku ambayo atafikishwa mahakamani.

Bireete, ni wakili na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo Kikuu cha Katiba na Uongozi (CCG) amekuwa akikosoa hotuba za Rais Museveni na baadhi ya sera za utawala wake.

Hasa amekuwa akikashifu vikali kuendelea kuzuiliwa kwa wanasiasa wa upinzani na mateso wanayoyapitia dhidi ya maafisa wa usalama.

CCG bado haikuwa imezungumzia kukamatwa kwa Bireete.

Uchaguzi wa Januari utawakutanisha Museveni, 81, ambaye amekuwa mamlakani tangu 1986 dhidi ya Mwimbaji mwanasiasa Bobi Wine.

Wine, 43, na chama chake cha NUP, wamekuwa wakilalamika kuwa wafuasi wao wamekuwa wakinyakwa na kuzuiliwa katika msafara wao wa kampeni.

Amelalamika mara si moja kwamba wafuasi wake wamekuwa wakiandamwa na vikosi vya usalama lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kukomesha matukio hayo.

Mwezi uliopita Mkuu wa UN kuhusu Haki za Kibinadamu Volker Turk pia alilalamikia ukandamizaji na kuandamwa kwa viongozi wa upinzani. UN ililalamikia kukamatwa na kuzuiliwa kwa zaidi ya wafuasi 550 wa upinzani.

Kiongozi mwengine wa upinzani Kizza Besigye anaendelea kusota gerezani zaidi ya mwaka moja tangu akamatwe na kushtakiwa kwa uhaini.