Habari Mseto

KFCB yatisha kupiga marufuku maonyesho ya wasanii wenye hulka ya Akothee

February 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

BODI ya Uanishaji wa Filamu nchini (KFCB) imeonya kupiga marufuku maonyesho yote ya wasanii katika umma ikiwa hawatafuata kanuni na maadili.

Wakati wa mkutano na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa KFCB Dkt Ezekiel Mutua bodi hiyo itawakamata na kuwafungulia mashtaka wasananii watakaokiuka sheria na kuchochea upotovu katika jamii.

“Ingawa bodi hii inatambua uhuru wa kusema, hatutaruhusu sanaa kutumiwa kama njia ya kuharibu utamaduni wetu au kuchochea tabia mbaya,” alisema na kuongeza kuwa wasanii hawataruhusiwa kuonyesha ‘ponografia’ hadharani.

“Watakaotaka kutoa nguo, watatakiwa kuchukua leseni ya kuvua nguo katika maonyesho,” alisema Dkt Mutua.

Aliongeza pia bodi hiyo itafunga klabu, hoteli au disko zinazokubalia kwasanii kukiuka sheria kwa kutumia maneno machafu au kuigiza kwa namna chafu.

“Bodi hii inashirikiana na Wizara ya Ndani, polisi na taasisi zingine za serikali kuhakikisha kuwa hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya hoteli au klabu zinazokiuka sheria, hasa zile zinarihusu watoto kuhudhuria shoo za watu wazima,” alisema.

KFCB imeamua kubuni masharti mapya kwa maeneo ambako maonyesho ya watu wazima yanaonyeshwa kulinda watoto, alisema mkurugenzi huyo.

Bodi hiyo ililazimika kuchukua hatua baada ya kile ilichosema kilikuwa ni ongezeko la malalamishi kutoka kwa umma kuhusiana na shoo chafu kwa baadhi ya wasanii ‘maarufu’.

Hii ni baada ya video ‘chafu’ ya msanii ‘Akothee’ (Esther Akoth) kusambazwa mitandaoni, “Ingawa bodi hii inaunga mkono ubunifu, inahofia dhana kwamba maudhui ya ngono au kuonyesha sehemu za siri au uchi huvutia wasikilizaji au watazamaji.”

Dkt Mutua alisema shoo zote ambazo zinachochea upotovu wa maadili katika jamii hasa kwa vijana wa umri mdogo hazitapewa leseni.

Hata hivyo, aliwataka wazazi kuwafunza watoto wao maadili na kuwazuia kuingia katika mitandao ya kijamii na intaneti kwa lengo la kuwalinda dhidi ya madhara ya matumizi ya intaneti.