Wanne wahofiwa kufunikwa na jengo lililoporomoka South C
Watu wanne, wakiwemo wawili waliokuwa wakitembea kwa miguu na walinzi wawili, wanahofiwa kufariki baada ya jengo la ghorofa 14 lililokuwa likijengwa kuporomoka jana asubuhi katika mtaa wa South C, Nairobi.Dereva wa teksi aliyeshuhudia alisema watu hao walikuwa eneo la ujenzi muda mfupi kabla ya jengo hilo kuporomoka.
Dereva huyo pia alijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali ya Mbagathi ambako anaendelea kutibiwa.
Kikosi cha maafisa wa kushughulikia Dharura kutoka Kaunti ya Nairobi, Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Majanga na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya kiliwasili eneo la tukio na uokoaji ulikuwa ukiendelea hadi tulipoenda mitamboni jana jioni.
Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku alisema serikali itachukua hatua dhidi ya waliohusika kuidhinisha na kujenga jengo hilo, akiongeza kuwa uchunguzi tayari umeanza.