Shinikizo zaibuka zikitaka Joho achukue wadhifa wa Oburu ODM
MAPAMBANO mapya ya kisiasa yanatokota katika Chama cha ODM, baada ya viongozi wa Pwani kusisitiza Waziri wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Hassan Joho, apewe wadhifa wa kiongozi wa chama.
Waziri Joho aliitisha hafla Jumatano kusherehekea miaka 81 tangu kuzaliwa kwa aliyekuwa kinara wa ODM, hayati Raila Odinga, katika eneo la Kikambala, Kaunti ya Kilifi.
Sherehe hizo zilibadilika kuwa mkutano wa kisiasa kuonyesha malengo yake ya usoni.
Viongozi wa kisiasa waliohutubu walimshinikiza waziwazi Bw Joho kuendea nafasi ya juu ndani ya chama, au kuwaleta viongozi wa Pwani pamoja chini ya chama kipya ambacho yeye atakiongoza.
Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, alisema eneo la Pwani lina ushawishi mkubwa ndani ya ODM, akimwomba Bw Joho kutumia mamlaka yake na ushawishi kuongoza chama.
Akilinganisha hali ya sasa chamani na mgawanyiko uliosababisha ODM kutengana na ODM-Kenya mnamo 2007, Bw Mung’aro alisema Pwani itapigania kutambulika ndani ya chama.
“Malizana na hawa watu na uchukue chama, hatutaki nusu yake. Hatutachukua sehemu A au B bali chama asili kwa sababu sisi pia tunastahili,” alisema.
Hali hii imejiri wakati chama kimekumbwa na mizozo ndani yake, huku upande mmoja ukimuunga mkono Rais William Ruto kwa muhula wa pili ifikapo 2027 na wengine wakipinga serikali ya Kenya Kwanza.
Bw Joho, aliyekuwa gavana wa Mombasa ambaye pia alihudumu kama naibu kiongozi wa ODM, ni miongoni mwa wanaounga mkono Rais Ruto.
Kauli za Bw Mung’aro ziliungwa mkono na aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, ambaye hivi majuzi alihama chama cha United Democratic Alliance (UDA) na kujiunga na Pamoja African Alliance (PAA).
Bi Jumwa alisema Bw Joho ana fursa nzuri ya kuwakilisha eneo la Pwani kitaifa akiwa kiongozi wa chama.
Alisisitiza kwamba, waziri huyo anapaswa kuchukua nafasi ya Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga, kama kiongozi wa ODM, akiwahimiza wanasiasa wa eneo hilo kuunga mkono hatua hiyo na kuwa tayari kuchukua njia tofauti ya kisiasa iwapo watashindwa.
“Kama chama cha ODM hakiwezi kupewa Waziri Hassan Joho, sisi kama Wapwani tunahitaji kuchukua njia tofauti ya kisiasa. Joho, una haki na uwezo wa kuwa kiongozi wa chama nchini,” alisema.
Viongozi wa Pwani walisema pia hawatakubali chochote chini ya nafasi ya Naibu Rais wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Ilibainika kuwa, lengo lao la kumhimiza Bw Joho kuwa kiongozi wa chama ni kumfanya atumie ushawishi wake kupigania nafasi hiyo kabla ya 2027.
Mnamo 2022, wanasiasa kadhaa walifanikiwa kufikia makubaliano na UDA chini ya muungano wa Kenya Kwanza, jambo lililowawezesha kupata nafasi za juu serikalini kwa sababu ya kuwa viongozi wa vyama.
Miongoni mwao ni Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi (PAA), Mwenyekiti wa Bunge la Kitaifa, Bw Moses Wetang’ula (Ford-Kenya), na Mkuu wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi, ambaye baadaye aliunganisha chama chake cha Amani National Congress (ANC) na UDA mwaka jana.
“Sharti letu la chini kabisa ni Naibu Rais, sio mwaka wa 2032 bali 2027. Kama ODM itafanya makubaliano yoyote na Rais William Ruto basi tunataka Naibu Rais atoke Pwani,” alisema Mbunge wa Garsen, Bw Ali Wario.
Mbunge Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Kilifi, Bi Gertrude Mbeyu, pia alisisitiza Bw Joho anafaa kupigania nafasi yake ndani ya ODM kwani alikuwa rafiki wa karibu na mshirika wa Raila.
Wanasiasa walisisitiza kuwa, uhusiano wao na Raila wakati alikuwa kiongozi wa ODM ulikuwa wa kipekee, na kwa hivyo Pwani inafaa kupewa nafasi ya juu chamani.
“Raila Amollo Odinga alituelewa na sisi tumemuelewa, alitupa tulichotaka na tulimpa kwa kurudisha, lakini sasa kwa kuwa hayupo hatuwezi kumilikiwa na mtu mwingine. Imani zetu haziwezi kumilikiwa tena na mtu yeyote,” alisema Mbunge wa Kaloleni, Bw Paul Katana.
Ingawa Bw Joho anahimiza eneo la Pwani kuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili, aliweka wazi kwamba eneo hilo lina uhusiano thabiti na marehemu Raila.
Alionyesha kuwa yuko tayari kuchukua uongozi wa ODM, akiwahimiza viongozi kutoka vyama vingine walioonyesha nia ya kutaka kumfuata wawe tayari kujiunga na chama.
“Sisi ni ODM na ODM ni sisi. Kwa hivyo wale wanaosema wataniunga mkono nitakapochukua uongozi wa chama wanapaswa kuanza kupanga hatua zao,” alisema.
Viongozi pia walihimiza eneo hilo kuungana kisiasa ili kulinda maslahi ya jamii ya Pwani.
Katika chaguzi zilizopita, ODM ilifanikiwa kuunganisha viongozi wa Pwani chini ya chama kimoja, ikishinda viti vingi kisiasa hadi migawanyiko ilipoathiri matokeo 2022 wakati baadhi ya viongozi wake wa zamani walipounga mkono Kenya Kwanza.