KCSE 2025: Matokeo kuangaliwa kupitia tovuti ya KNEC sio SMS
BARAZA la Kitaifa la Mtihani Kenya (KNEC) Ijumaa, Januari 9, 2026 lilitoa rasmi matokeo ya Mtihani wa KCSE wa mwaka 2025.
Tofauti na miaka iliyopita, watahiniwa hawataweza kupata matokeo yao kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS).
Badala yake, matokeo hayo yatapatikana mtandaoni pekee kupitia tovuti ya KNEC.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Waziri wa Elimu, Julius Migos Ogamba, alisema kuwa watahiniwa wataweza kuangalia matokeo yao kupitia tovuti ya KNEC au moja kwa moja kwa https://results.knec.ac.ke/
“Kila mtahiniwa atahitajika kuweka nambari yake ya mtihani (index number) na jina lake moja lililosajiliwa,” alisema Bw Ogamba.
Baada ya kuweka taarifa hizo, watahiniwa wanapaswa kukubali masharti ya faragha na ruhusa ya matumizi, kisha wabonyeze kitufe cha kutafuta (search) ili kuona matokeo yao.
Matokeo hayo yaliwekwa kwenye tovuti hiyo mara moja baada ya kutangazwa rasmi na Waziri wa Elimu katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Upili ya AIC Chebisas, mjini Eldoret.
KNEC imewahimiza watahiniwa na wazazi kuwa watulivu wanapofikia mfumo huo mtandaoni, hasa kutokana na idadi kubwa ya watu wanaotarajiwa kuutumia kwa wakati mmoja.