Kimataifa

Museveni atangaza Sikukuu ya siku mbili tarehe za uchaguzi

Na BENSON MATHEKA January 10th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

RAIS wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni ametangaza Januari 15 na 16, 2026 kuwa sikukuu za kitaifa ili kuwapa raia muda wa kushiriki uchaguzi wa urais na wabunge wa taifa hilo utakaofanyika wiki ijayo, baada ya kipindi cha kampeni za urais zilizojaa mvutano.

Tangazo hilo lilitolewa na Rais Museveni kupitia Notisi ya Kisheria chini ya Sheria ya Sikukuu za Umma, Sura ya 174, na kuchapishwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali.

“Kwa kutekeleza mamlaka niliyopewa na Kifungu cha 2(2) cha Sheria ya Sikukuu za Umma, natangaza tarehe 15 na 16 Januari, 2026 kuwa sikukuu za kitaifa kote Uganda kwa madhumuni ya kuwawezesha wananchi kushiriki uchaguzi wa Rais na Wabunge,” ilisema sehemu ya notisi hiyo.

Serikali ilisema mapumziko hayo ya siku mbili yanalenga kuwawezesha wapiga kura kote nchini kusafiri, kupanga foleni na kupiga kura bila vikwazo vya majukumu ya kikazi.

Sikukuu hizo zitatekelezwa kitaifa na zitahusu taasisi za umma na za kibinafsi, huku Uganda ikijiandaa kwa uchaguzi unaotarajiwa kufuatiliwa kwa karibu sana.

Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka wa 1986, anawania muhula mwingine, huku uchaguzi huo pia ukiamua muundo wa Bunge la Uganda.

Takribani wapiga kura21.6  milioni  waliojiandikisha watashiriki chaguzi tatu tofauti: uchaguzi wa rais, uchaguzi wa wabunge 353 wa maeneo bunge, pamoja na uteuzi wa wawakilishi wanawake 146, mmoja kutoka kila wilaya.

Rais Museveni na kiongozi wa upinzani Bobi Wine ndio wagombea wakuu wa urais, huku huu ukiwa mtanange wao wa pili kwenye sanduku la kura.

Museveni, mwenye umri wa miaka 81, alishinda uchaguzi wa 2021 kwa kupata asilimia 58 ya kura dhidi ya asilimia 35 za Bobi Wine, kura iliyogubikwa na madai ya wizi wa kura na ukandamizaji mkubwa wa upinzani.

Kwa mujibu wa sheria za Uganda, mgombea wa urais lazima apate asilimia 50 pamoja na kura moja ili kuepuka duru ya pili ya uchaguzi katika mfumo wa kura wa awamu mbili, huku Waganda wengi wakiendelea kueleza wasiwasi wao kuhusu uaminifu wa mchakato wa uchaguzi.

Uchaguzi wa Uganda unafanyika takribani miezi minne baada ya nchi jirani ya Tanzania kufanya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali, uliosababisha vurugu baada ya matokeo kutangazwa katika baadhi ya maeneo.

Rais Samia Suluhu alitangazwa mshindi baada ya matokeo yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Tanzania mnamo Jumamosi, Novemba 1, kuonyesha kuwa alipata kura milioni 31.9, sawa na asilimia 97.66 ya kura zote zilizopigwa.