JUMLA ya wanafunzi 232,281 waliofanya Mtihani wa Darasa la nane (KCPE) mwaka wa 2021 hawakufanya mtihani wa kidato cha nne (KCSE), kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Wizara ya Elimu.

Takwimu za Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini (KNEC) zinaonyesha kuwa watahiniwa 1,225,507 walifanya mtihani wa KCPE mwaka wa 2021.

Hata hivyo, ni wanafunzi 993,226 pekee waliofanya mtihani wa KCSE mwaka wa 2024, hali inayoangazia kiwango kikubwa cha wanafunzi wanaokatiza masomo katika ngazi ya sekondari.

Takwimu zaidi kutoka KNEC zinaonyesha kuwa watahiniwa 2,634 walijisajili lakini hawakufanya mtihani wa KCSE mwaka wa 2025.

Kwa jumla, watahiniwa 995,860 walikuwa wamejisajili kufanya mtihani wa kitaifa wa sekondari, lakini ni 993,226 pekee waliojitokeza kufanya mtihani.

Takwimu hizi zinaonyesha ongezeko thabiti tangu mwaka wa 2021, ambapo watahiniwa 830,854 walisajiliwa na 826,807 wakafanya mtihani.

Serikali imeendelea kutekeleza sera asilimia 100 ya wanafunzi kujiunga na sekondari, inayosisitiza kuwa kila mtoto ajiunge na shule ya msingi na kukamilisha masomo ya sekondari.

Sera hii inatokana na Sheria ya Elimu ya Msingi, inayowalazimu wazazi wote raia wa Kenya au wale ambao watoto wao wanaishi nchini kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya sekondari.

Ingawa sera hii ina nia njema, inahitaji kufanyiwa mabadiliko ili kushughulikia masuala halisi yanayoibuliwa na wazazi, wanafunzi wenyewe na wadau wa elimu. Sio wanafunzi wote wanaofaa mfumo rasmi na mgumu wa elimu ya sekondari, na wengi wangependelea, baada ya shule ya msingi, kufuata kozi za ufundi kama useremala, ushonaji, uashi na nyinginezo.

Wanafunzi kama hao wanapaswa kuruhusiwa kufuata mkondo huo, huku wakiendelea kufundishwa masomo kama Kiingereza na Hisbati ili kuboresha ujuzi wao mawasiliano na ujasiriamali.

Wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya KCSE 2025, shule za kitaifa ziliongoza kwa kutoa wanafunzi waliopata matokeo bora, na hivyo kudumisha sifa yao kama vituo bora kwa elimu.

Kati ya watahiniwa 1,932 waliopata A kamili, wanafunzi 1,526 (asilimia 79) walitoka shule za kitaifa. Shule za mikoa zilifuata kwa wanafunzi 197, huku shule za kibinafsi zikiwa na 185 waliopata alama ya juu.

Shule za kaunti ndogo zilifanya vyema kuliko shule za kaunti kwa kutoa wanafunzi 72,699 waliojiunga na vyuo vikuu ikilinganishwa na 36,600 wa shule kiwango cha kaunti, hali inayoonyesha uwezo mkubwa wa shule ndogo zilizo nje ya mfumo wa shule za kifahari.