Habari

Kanchory kwa Junet: Acha Baba aendelee kupumzika kwa amani

Na BENSON MATHEKA January 11th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA ajenti mkuu wa Azimio katika uchaguzi wa urais 2022, Saitabao Ole Kanchory, amesema kuwa endapo aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga angekuwa hai leo, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed asingekuwa akizungumza namna anavyofanya kwa sasa.

Akizungumza katika mahojiano Jumatano, Januari 7, 2025, Kanchory, ambaye amekuwa akikosoa viongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) wanaounga mkono serikali jumuishi, alisema Junet na mawaziri waliokuwa viongozi wa ODM wanamsaliti Raila akiwa kaburini kutoka na mvutano unaoshuhudiwa ndani ya chama hicho.

Kulingana na Bw Kanchory, jambo linalomuumiza zaidi ni mienendo ya viongozi waliokuwa karibu na Raila, akiwemo Junet Mohamed, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na Waziri wa Fedha John Mbadi tangu kifo chake.

Alisema viongozi hao wanaendesha siasa zinazokiuka misingi na maono ya Raila Odinga, akiongeza kuwa kama Raila angekuwa hai leo, wangekuwa wakizungumza kwa tahadhari zaidi na kuonyesha uwajibikaji.

Kanchory alisisitiza kuwa endapo Raila angefufuka kutoka kaburini, angewafuta kazi viongozi hao mara moja, hasa wale waliojiunga na serikali chini ya muafaka wake na Rais William Ruto.

Alidai kuwa Mbadi, Wandayi na Junet wametumia vibaya nyadhifa walizoaminiwa na Raila kwa manufaa yao binafsi badala ya maslahi ya taifa, kinyume na alichosimamia kiongozi huyo marehemu.

Kauli hizi zinajiri wakati ambapo ODM inakumbwa na migogoro ya ndani, huku Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna akilaumiwa vikali kwa kupinga wanaounga azma ya Rais William katika uchaguzi wa 2027.

Chama hicho kimegawanyika kuhusu mwelekeo wake baada ya Raila. Sifuna amesisitiza kuwa ODM inapaswa kusimamisha mgombeaji wa urais kumpinga Rais Ruto, akisema hata yeye ana sifa za kuwania wadhifa huo.

Hata hivyo, kiongozi wa chama Oburu Odinga amedai kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama, kiongozi wa chama ndiye mgombeaji rasmi wa urais.

Junet Mohamed aliunga mkono kauli hiyo, akisema Oburu ndiye msemaji na mbeba bendera wa chama kwa sasa, na mwenye mamlaka ya kuamua masuala ya uteuzi wa mgombeaji wa urais.