Dalili Matiang’i anajipanga kivyake
DALILI zinaendelea kujitokeza kuwa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, anaweza kujitenga na muungano mpana wa upinzani na kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027 kwa tiketi ya chama cha Jubilee, hatua inayoweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa siasa za upinzani nchini.
Haya yanajiri huku Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, akichukua msimamo mkali dhidi ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akimshambulia kwa kudai Mlima Kenya unastahili kuwa na chama kimoja kikuu cha kisiasa.
Bw Matiang’i anategemea kwa kiwango kikubwa kura za eneo la Mlima Kenya ambako mlezi wake kisiasa na kiongozi wa Jubilee Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ana umaarufu.
Akizungumza katika mahojiano na Spice FM, wiki hii, Kioni alitaja kauli za Gachagua kama za kurudisha nyuma demokrasia na akisema zinakiuka Katiba ya Kenya inayolinda mfumo wa vyama vingi.
“Nilimsikia mtu akisema eneo hili litakuwa na chama kimoja pekee. Hiyo ni kauli ya kurudisha nyuma nchi na ni kinyume na Katiba,” alisema Kioni.
Kioni alionya kuwa kauli za aina hiyo zinaweza kuleta mpasuko mkubwa ndani ya upinzani na hata kulazimu Jubilee kuchukua mkondo wake wa kisiasa.
“Tulipigania Katiba hii. Sitatoa kafara mustakabali wangu wa kisiasa kwa sababu ya kauli zinazotolewa ovyo. Nikiendelea kusikia maneno kama hayo, nitaondoka na nitafuata njia yangu,” aliongeza.
Kauli za Kioni zimechukuliwa na wachambuzi wa siasa kama ishara wazi ya Jubilee kujitenga polepole na muungano wa upinzani unaohusishwa na Gachagua, huku chama hicho kikimjenga Matiang’i kama mgombea wake wa urais.
Chama hicho, kinasisitiza kuwa kingali ndani ya muungano wa upinzani.
Wakati huo huo, Dkt Matiang’i, ambaye ni Naibu Kiongozi wa Jubilee, amekuwa akionekana hadharani zaidi na kufanya mikutano ya kisiasa, jambo linaloashiria maandalizi ya kampeni kitaifa.
Hata hivyo, hali hii haijapokelewa vyema na baadhi ya watu wanaomuonya dhidi ya kutegemea Uhuru kufanikisha azma yake ya urais.
Katibu Mkuu wa COTU, Francis Atwoli, alimtahadharisha Matiang’i dhidi ya kutegemea mno uungwaji mkono na Uhuru Kenyatta, akisema historia inaonyesha Uhuru alishindwa kumfikisha Raila Odinga Ikulu licha ya kumuunga mkono akiwa rais.
“Kama Uhuru hakuweza kumfanya Raila awe Rais, Matiang’i akijiamini sana, atajipata pabaya,” alisema Atwoli.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa huenda Dkt Matiang’i akachochewa kujitenga na muungano wa upinzani kutokana na kura ya maoni inayomuonyesha akishinda vinara wengine kwa umaarufu.
Kura ya maoni ya Infotrak wiki jana inaonyesha Matiang’i kama mpinzani wa karibu zaidi wa Rais William Ruto kuelekea 2027.
Kulingana na kura hiyo, Ruto anaongoza kwa asilimia 28 huku Matiang’i akifuata kwa asilimia 13.
Vinara wengine wa upinzani waliotajwa ni Kalonzo Musyoka (12), Rigathi Gachagua, Martha Karua na David Maraga, waliopata asilimia kati ya tano na mbili. Asilimia 31 ya Wakenya bado hawajaamua watamuunga mkono nani.
Mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema kinachoonekana kama umaarufu wa Matiang’i kinaweza kumponza asipofanya maamuzi ya busara na kuungana na wenzake katika upinzani.
“Matiang’i anakumbukwa kwa nidhamu na uthabiti wake kama afisa wa serikali na sio mwanasiasa. Bila muungano mpana wa upinzani, safari yake itakuwa ngumu,” anasema Dkt Gichuki.
Anasema iwapo ataamua kuwania kwa tiketi ya Jubilee atagawanya kura za upinzani lakini huenda matarajio yake katika Mlima Kenya yasitimie.
“Upinzani ukigawanyika, utampa Ruto nafasi kubwa ya kushinda muhula wa pili. Lakini huenda Matiang’i akashangaa sana kwa kuwa Mlima Kenya unaweza kwenda kinyume na juhudi zozote za kugawanya kura kwa lengo la kumbandua Ruto” anasema.
Huku hali ikiwa tete, macho yote sasa yanaelekezwa kwa hatua atakayochukua Matiang’i ikiwa ataendelea kusukuma ajenda ya Jubilee pekee au atajaribu kusuka upya muungano wa upinzani ili kuipa serikali ya Kenya Kwanza changamoto kubwa 2027
Wachambuzi wanasema dalili za Matiang’i zinaonekana katika mkakati wa Jubilee wa kujijenga upya hasa katika Mlima Kenya ambako kuna vyama vingine ikiwemo DCP ya Bw Gachagua eneo ambalo kulingana na kura ya maoni ya Infortrak, asilimia 36 ya wapiga kura ambao bado hawajafanya uamuzi wa mwisho.
Kwa sasa, vinara wengine wa upinzani akiwemo Gachagua, Kalonzo Musyoka, Martha Karua, Eugene Wamalwa, Justin Muturi na George Natembeya wanasisitiza kuwa wamejitolea kuungana katika uchaguzi mkuu wa 2027 huku wachambuzi wakisema huo ndio mtihani wao mkubwa.
Dkt Matiang’i amekuwa akikutana na baadhi ya vinara wa upinzani bila Gachagua, Muturi, Kalonzo na Wamalwa hatua inayoonekana kama ya kujenga mrengo wake kivyake.
Dkt Matiang’i amekuwa akipuuza madai kuwa muungano huo unagawanyika akisema kusuka muungano wa vyama vingi sio rahisi na lazima kuwe na tofauti za maoni japo kauli za washirika wake zinaonyesha anajipanga kivyake kupitia Jubilee.