Iran yaapa kulipiza kisasi iwapo Amerika itaipiga
TEHRAN, IRAN
TEHRAN ilitishia Jumapili kulipiza kisasi dhidi ya ngome za kijeshi za Israel na Amerika endapo Amerika itashambulia Iran, onyo lililotolewa huku duru za Israel zikisema taifa la Kiyahudi limemakinika kuhusu uwezekano wa Amerika kuingilia kati kwa namna yoyote.
Huku utawala wa kidini Iran ukikabiliwa na maandamano makubwa zaidi ya kupinga serikali kuwahi kutokea tangu 2022, Rais Donald Trump ametishia mara kwa mara kuingilia kati katika siku za hivi karibuni na kuwaonya watawala wa Iran dhidi ya kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji.
Jumamosi, Trump alisema Amerika imesimama “tayari kusaidia”.
Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf, akizungumza bungeni Jumapili, alionya dhidi ya “kosa la kimaamuzi”.
“Tuwe wazi: endapo shambulizi litatekelezwa dhidi ya Iran, maeneo yaliyo na watu (Israel) pamoja na ngome na meli za Amerika zitakuwa zetu za kulenga kihalali,” alisema Qalibaf, kamanda wa zamani katika kikosi maalum cha jeshi la Iran, Revolutionary Guards.
Serikali imezidisha juhudi za kuzima machafuko ambayo yamezagaa kote Iran tangu Desemba 28. Maandamano hayo yalianza kuhusiana na ongezeko la mfumko wa bei, kabla ya kugeukia utawala wa kidini ambao umeongoza tangu Mageuzi ya Kiislamu ya 1979.
Serikali imeshutumu Amerika na Israel kwa kusababisha ghasia.
Duru za Israel zilizohudhuria mashauriano kuhusu usalama wa Israel wikendi, zilisema taifa hilo la Kiyahudi limekaa chonjo lakini hazikufafanua maana yake.
Israel na Iran zilipigana vita vilivyodumu siku 12 mnamo Juni, ambapo Amerika iliungana na Israel kutekeleza mashambulizi ya angani.
Iran ilijibu mashambulizi hayo kwa kufyatulia makombora ngome ya angani ya Amerika nchini Qatar.
Jeshi la Revolutionary Guards mnamo Jumamosi lilishutumu “magaidi” kwa kushambulia vituo vya usalama.
Mkuu wa polisi, Ahmad-Reza Radan, alisema vikosi vya usalama vimeimarisha juhudi za kuwakabili “wanaozua ghasia.”
Watawala wa Iran wamezima mawimbi ya awali ya machafuko, ikiwemo majuzi, 2022, kuhusu kifo kizuizini cha mwanamke aliyeshutumiwa kukiuka kanuni za mavazi.
Trump, akichapisha mtandaoni Jumamosi alisema: “Raia wa Iran wanakaribia uhuru, pengine kuliko walivyowahi kuwa hapo awali. Amerika imesimama tayari kusaidia!!!”
Kupitia mawasiliano ya simu Jumamosi, Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, na Waziri wa Usalama wa Ndani Amerika, Marco Rubio walijadili uwezekano wa Amerika kuingilia kati Iran, kulingana na duru za Israeli zilizohudhuria mazungumzo hayo.
Afisa wa Amerika alithibitisha wanaume hao wawili walizungumza lakini hakusema ni masuala yapi waliyojadili.
Afisa mkuu wa ujasusi Amerika Jumamosi alielezea hali nchini Iran kuwa “mchezo wa kustahimili.”
Upinzani ulikuwa unajaribu kushinikiza hadi viongozi wakuu serikali ama watoroke au kuhama kambi, huku mamlaka ikijaribu kupanda hofu ya kutosha kusafisha mitaa pasipo kupatia Amerika sababu yoyote ya kuingilia kati, alisema afisa.
Israeli haijaashiria kupenda kuingilia kati Iran huku maandamano yakikumba taifa hilo na kuzidisha taharuki kati ya mahasimu wawili wakuu kuhusu wasiwasi wa Israeli kwa miradi ya Iran ya nuklia na silaha za kivita.
Katika mahojiano na gazeti la Economist yaliyochapishwa Ijumaa, Netanyahu alisema kutakuwa na athari mbaya zaidi kwa Iran ikiwa itashambulia Israeli.
Akirejelea maandamano, alisema: “Kila mtu, nafikiri tunapaswa kuona kinachoendelea ndani ya Iran.”