Trump asisitiza lazima atie adabu Iran
WASHINGTON, Amerika
RAIS wa Amerika Donal Trump amesema nchi yake inapania kuchukua “hatua kali” dhidi ya Iran kwa kuwashambulia waandamanaji wanaopinga serikali hiyo; ikiwemo hatua za kijeshi.
“Tunalishughulikia suala hilo kwa makini. Jeshi letu linalifuatilia na tunatafakari kuchukua baadhi ya hatua kali. Tutafanya uamuzi hivi karibuni,” akawaambia wanahabari Jumapili jioni akiwa kwenye ndege yake rasmi ya Air Force One, akiwa safarini kutoka Florida akielekea Washington.
Trump alisema kuwa uongozi wa Iran umempigia simu ukitaka “tufanye mazungumzo” baada ya tishio lake kwamba angeamuru wanajeshi wa Amerika kuishambulia nchi hiyo.
Rais huyu wa Amerika alieleza kuwa mkutano wa mazungumzo unapangwa lakini huenda jeshi la Amerika likachukua hatua dhidi ya Iran hata kabla ya mkutano huo kufanyika.
Utawala wa Iran haukutoa jibu mara moja kuhusiana na tishio hilo la Amerika.
Lakini mnamo Jumapili asubuhi, viongozi wa Iran walionya vikali dhidi ya mpango wa Amerika kuchukua hatua za kijeshi dhidi yake huku Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf akisema hivi: “Endapo Iran itashambuliwa, tutalenga himaya zote zilizotwaliwa (Israeli).”
Pia Spika huyu alisema kuwa Iran ingeshambulia vituo vyote vya kijeshi vya Amerika na meli zao.
Maandamano nchini Iran yalianza mnamo Desemba 28, 2025 wakati wafanyabiashara katika jengo la kibiashara la Grand Bazaar lililoko jijini Tehran walifunga maduka yao wakilalamikia kushuka kwa thamani ya sarafu wa Iran, Rial.
Maandamano huyo yalienea haraka kote nchini humo huku malalamishi yakiwa kupanda kwa gharama ya maisha na utawala mbaya wa kidini nchini Iran.
Iran imetawaliwa na viongozi wa kidini tangu Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanyika mnamo 1979.
Kulingana na shirika la habari la kitaifa nchini Iran, jumla ya walinda usalama 109 wameuawa katika makabiliano na waandamanaji.
Lakini wanaharakati wa upinzani walioko nje ya Iran wanadai idadi ya waliokufa ni juu wakiwemo mamia ya waandamanaji.
Mawasiliano ya intaneti pia yamezimwa kwa zaidi ya saa 72, kulingana na makunda ya kufuatilia ghasia hizo.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alisema Jumapili kwamba serikali yake iko tayari kuwasikiza waandaamanaji lakini akawataka wananchi kuwadhibiti watu wenye nia ya kuzua uharibifu pamoja na magaidi ili wasiharibu nchi yetu.”
Aliambia shirika la habari la IRIB kwamba Israel na Amerika, walianzisha vita vya siku 12 dhidi ya Iran mnamo Juni mwaka jana, ndizo zinachochea fujo nchini mwake.
Akaeleza: “Wale ambao walishambulia nchi yetu ndio wanajaribu kuchochea fujo huku majadiliano yakiendelea kuhusu namna ya kuimarisha uchumi.”
Machafuko yanashuhudiwa Iran wakati ambapo Rais Trump anatekeleza sera kali za kigeni, baada ya kumkamata Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.
Kesho, Jumanne, Trump ameratibiwa kukutana na washauri wakuu kujadili hatua za kuchukua dhidi ya Iran, afisa mmoja wa Amerika aliwaambia wanahabari.
Jarida la Wall Street liliripoti kwamba hatua hizo zinajumuisha mashambulio ya kijeshi, matumizi ya silaha za kidijitali, kupanualiwa kwa vikwazo dhidi ya Iran na kutoa usaidizi mitandaoni kwa wapinzani wa serikali.