Bobi Wine: Nimeteswa ya kutosha ila sitakufa moyo, lazima Museveni aondoke
KAMPALA, UGANDA
MWANASIASA maafuru ambaye ni mpinzani mkuu nchini Uganda, Bobi Wine, amesema amepigwa na kushambuliwa kwa vitoa machozi na kumwagiwa maji ya pilipili alipokuwa akiendesha kampeni zake za kumpinga Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986.
Wine, mwenye umri wa miaka 43 amesema vurugu hizo hazimshangazi, kwani zimekuwa sehemu ya safari yake ya kisiasa kwa karibu muongo mmoja.
Ingawa wachambuzi wengi hawampi nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi wa Alhamisi dhidi ya Museveni, ambaye ana umri wa miaka 81, Wine ameibuka kuwa mpinzani wake mkuu kwa kuhamasisha mamilioni ya vijana waliokata tamaa.
Hii ni mara yake ya pili kuwania urais, wakati huu kukiwa na dalili kuwa Museveni anapanga hatima ya urithi wa madaraka.
“Kila mara tunapopita mazingira haya hatari na kufika kwa wananchi, tunahisi kama pumzi ya maisha mapya,” Wine aliambia shirika la habari la Reuters mwezi huu.
“Tunajua kuwa serikali inafanya haya kutuvunja moyo, lakini tunaamua kuendelea mbele kuonyesha kuwa hatuwezi kuzimwa.”
Serikali ya Uganda, hata hivyo, imesema vikosi vya usalama viliingilia kati tu pale wafuasi wa Wine walipokiuka masharti ya kampeni, kama vile kuziba barabara au kufanya mikutano nje ya muda ulioruhusiwa.
Museveni mara kwa mara amempuuza Wine, akisema anafadhiliwa na mataifa ya kigeni, yakiwemo madai kuwa anahamasisha ushoga.
Katika uchaguzi wa 2021, Wine alimkabili Museveni katika kura zilizokumbwa na mauaji ya zaidi ya wafuasi 50 wa upinzani, madai ya udanganyifu na kukamatwa mara kadhaa kwa mgombea huyo wa upinzani.
Alilazimika kuvaa koti la kuzuia risasi na kofia ya chuma wakati wa kampeni.
Baadaye aliondoa kesi ya kupinga matokeo yaliyompa Museveni asilimia 58 ya kura, akidai mahakama ilikuwa na upendeleo.
Amerika ilisema uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki, madai yaliyokanushwa na serikali ya Uganda.
Katika kampeni za sasa, vikosi vya usalama vimeripotiwa kufyatua risasi na vitoa machozi katika mikutano ya Wine, hali iliyosababisha kifo cha angalau mtu mmoja na kukamatwa kwa mamia ya wafuasi wake.