Adrien Rabiot athubutu kumfuta kazi mama yake hasa
Na MASHIRIKA na GEOFFREY ANENE
NYOTA wa Paris Saint-Germain, Adrien Rabiot amepiga kalamu wakala wake Veronique Rabiot, ambaye ni mamake, baada ya uhamisho wake hadi Barcelona nchini Uhispania kugonga mwamba.
Akisalia na miezi sita pekee katika kandarasi yake na mabwanyenye wa PSG, kiungo huyu alionekana kuwa pua na mdomo kutua uwanjani Camp Nou kwa Sh4,537,904,932.
Hata hivyo, uhamisho huo uligonga ukuta pale wakala wake alipokosa kukamilisha mazungumzo hayo.
Tovuti ya talkSPORT inasema kwamba mama Veronique aliahidi mwanawe Adrien ataangalia ofa ya Barcelona tena ili kukamilisha yote yaliyohitajika kufanikisha uhamisho huo, lakini hakutimiza ahadi yake.
Ripoti nchini Ufaransa sasa zinasema Adrien, 23, ameachisha kazi mamake na kuajiri wakala mwingine akitumai atafanikisha uhamisho mwisho wa msimu huu wa 2018-2019.
Adrien hajakuwa akichezeshwa na kocha Thomas Tuchel baada ya wawili hawa kukosana.
Mchezaji huyu sasa anachezea timu ya PSG ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 hadi mwisho wa msimu huu.