Tume ya Uchaguzi Uganda yaomba radhi kwa changamoto za upigaji kura
TUME ya Uchaguzi ya Uganda imeomba radhi kwa wapiga kura kufuatia changamoto za kiufundi zilizosababisha kuchelewa kuanza kwa zoezi la upigaji kura kote nchini.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa kijamii wa X, tume hiyo ilisema ililazimika kuwaagiza wasimamizi wa uchaguzi kutumia Sajili ya Kitaifa ya Wapigakura badala ya Vifaa vya Kielektroniki vya Kuthibitisha Wapiga Kura vya Biometric (BVVKs), vilivyokumbwa na hitilafu za kiufundi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa maafisa wa kiufundi wa tume wanaendelea kushughulikia changamoto zilizojitokeza, huku shughuli za upigaji kura zikiendelea baada ya kucheleweshwa kwa takribani saa nne.
Hata hivyo, baadhi ya wapiga kura wameripotiwa kuondoka katika vituo vya kupigia kura bila kupiga kura, wakieleza kutokuwa tayari kusubiri hitilafu hizo kutatuliwa au utekelezaji wa agizo jipya la kutumia Daftari la Taifa la Wapigakura.
Tume ya Uchaguzi haijabainisha iwapo saa za upigaji kura zitaongezwa ili kufidia muda uliopotea kutokana na ucheleweshaji uliosababishwa na changamoto za kiufundi.