Habari

Junet atoboa siri za Raila

Na JUSTUS WANGA Na SAMUEL OWINO January 17th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

KIONGOZI wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed, amejitetea vikali dhidi ya madai kuwa yeye ni broka wa kisiasa anayenuia kuuza chama cha ODM kwa Rais William Ruto.

Akizungumza kutoka ofisi yake katika majengo ya Bunge, Junet amesema madai hayo ni ya kupotosha na yanapuuza historia, misingi na uhalisia wa siasa za ODM.

Kwa msimamo mkali lakini wa utulivu, alisisitiza kuwa ODM si mali ya mtu binafsi, bali ni taasisi ya umma isiyoweza kuuzwa kwa mikataba ya siri au maamuzi ya mtu mmoja.

“ODM haiwezi kuuzwa. Ni chama cha wananchi. Kama kuingia mazungumzo ya kisiasa na chama kilichoko madarakani kunaitwa kuuza ODM, basi hiyo ni lugha ya kuwavunja moyo wale wanaotaka mazungumzo,” alisema Junet, akiongeza kuwa chama chake kitaendelea kutafuta mamlaka na nguvu za kisiasa kwa njia mbalimbali, ikiwemo majadiliano ya wazi.

Junet alifafanua kuwa uhusiano wa ODM na Rais Ruto ulijengwa kwa tahadhari na baada ya mashauriano ya ndani ya chama, akisema aliyekuwa kiongozi wa chama Raila Odinga ndiye aliyefungua njia ya mazungumzo hayo.

Alisema Raila alimuita na kumshirikisha katika mkutano muhimu na Rais Ruto, ulioweka msingi wa kuundwa kwa Serikali Jumuishi.

“Kulikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa nchi wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z. Raila alitaka utulivu wa taifa kwanza. Hakuwa na haraka ya kuingia serikalini, lakini alielewa kuwa hali ya nchi ilihitaji majadiliano ya haraka,” asema Junet.

Kwa mujibu wake, Raila alipendekeza kuwe na mkutano wa kitaifa Bomas uliowaleta pamoja viongozi wa kisiasa, vijana wa Gen Z na wadau wengine, lakini Rais hakuwa na muda wa kusubiri kwa kuwa nchi haikuwa na Baraza la Mawaziri.

Mbunge huyo wa Suna Mashariki alisema kulingana na Rais Ruto, hata Raila mwenyewe hakuwa salama iwapo maandamano ya Gen Z yangeendelea kutikisa nchi.

Hatimaye, walikubali kushirikiana, ingawa Raila aliingia katika mazungumzo kwa tahadhari kubwa.

Ni katika mchakato huo ndipo Oburu Oginga aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa jopo la ODM lililohusika na mazungumzo ya kisiasa.

Junet anasema Oburu alikuwa chaguo la asili la Raila kutokana na uzoefu, uaminifu na historia yake ndani ya chama.

“Kila mara Raila alipokutana na rais, mtu wa kwanza kumpigia simu alikuwa Oburu. Huyo ndiye alikuwa mshauri wake wa karibu zaidi. Oburu ana uzoefu, ana maarifa na ni ODM damu,” alisema Junet, akipuuzilia mbali hoja kuwa umri ni kikwazo kwa uongozi.

Alisema nguvu ya ODM haiko kwa mtu mmoja bali iko kwenye mifumo yake, hasa Kamati Kuu na Baraza la Kitaifa la Wajumbe (NDC).

Kwa mtazamo wake, migogoro ya sasa ndani ya chama inachochewa zaidi na kauli za watu binafsi kuliko misimamo rasmi ya chama.

“Raila hakuwahi kufanya uamuzi mkubwa bila kupitia vyombo vya chama. Alisikiliza kila mtu, akaandika kila hoja, kisha kuongoza kwa maridhiano. Huo ndio utamaduni aliotuachia,” alisema.

Kuhusu madai kuwa Raila alikuwa tayari kuacha azma ya urais 2027, Junet asema hilo si kweli.

Alifafanua kuwa Raila alikuwa bado anapanga kuwania urais, akiamini hakuna kiongozi mwingine katika upinzani aliyekuwa na uwezo wa kumshinda Rais Ruto.

“Alikuwa na mipango mingi. Angeunganisha upinzani wote chini ya tiketi moja. Kama asingegombea, angeimarisha ODM na kuingia serikalini rasmi.

Hata kulikuwa na wazo la kumshawishi Ruto kumuunga mkono 2027, kisha Ruto arudi 2032. Haya yote yalikuwa yaamuliwe mwaka huu wa 2026,” alisema Junet.

Junet alikanusha vikali madai kwamba ODM ilikuwa imeamua kumuunga mkono Rais Ruto moja kwa moja 2027, akisema uamuzi huo haujawahi kufanywa.

Alisema mazungumzo ya kisiasa ni mchakato unaoendelea na hakuna kinachofungwa mapema.

Sehemu nyeti zaidi ya mahojiano ilikuwa kuhusu madai ya pesa za kampeni za uchaguzi wa 2022.

Junet alifungua ukurasa ambao kwa muda mrefu umekuwa ukizungumzwa kwa chini chini, akisisitiza kuwa hakuwahi kula fedha za chama wala za maajenti wa uchaguzi.

“Nimekuwa kimya kwa heshima ya Raila. Aliniambia nisijibu madai hayo. Kama ningekuwa niliiba pesa za kampeni, Raila asingekuwa amenifanya Kiongozi wa Wachache baada ya uchaguzi,” alisema.

Kwa mujibu wa Junet, fedha za kulipa maajenti zilikuwa chini ya usimamizi wa kikosi cha kampeni ya upande wa Jubilee.

Alimtaja Muhoho Kenyatta, ndugu ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, kama aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya fedha, pamoja na Patrick Mburu ambaye alisimamia mfumo wa malipo.

“Patrick Mburu alituambia alikuwa na taarifa zote za maajenti kwenye kompyuta na angewatumia pesa kwa kubonyeza kitufe tu kupitia Safaricom. Tulielekezwa tuache suala la pesa za maajenti. Mimi sikushika hata shilingi,” alisema na kuongeza anaweza kuapa kwa Kuran kuwa hana hatia.

Aliongeza kuwa Raila alikuwa na fedha zake binafsi za kampeni, lakini suala la maajenti liliwekwa mikononi mwa kikosi cha Uhuru.

Junet alisema yuko tayari kwa ukaguzi wowote wa hesabu, akisisitiza kuwa ukweli utabaki kuwa ukweli.

Kuhusu aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, Junet alisema mchango wake katika siasa za ODM hauwezi kupuuzwa, lakini akadai kuwa baadhi ya migawanyiko ya sasa inahusishwa na shinikizo la kutaka ODM ibaki katika Azimio bila kuzingatia hali mpya ya kisiasa nchini.

Alidai Uhuru hakufanya juhudi za kutosha kuhakikisha Raila anashinda urais 2022, akisema “alikuwa na nguvu zote za vyombo vya dola lakini hakuzitumia kikamilifu.