Habari

Sitawatenga: Ruto arudi Mlimani kufufua ushawishi wake

Na GITONGA MARETE January 18th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto siku ya Jumamosi alizindua upya mkakati wa kisiasa wa kurejesha uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, akikita juhudi zake kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ushirikishaji wa wananchi mashinani.

Akizungumza katika Ikulu Ndogo ya Sagana, Kaunti ya Nyeri, mbele ya zaidi ya viongozi wa mashinani 17,000 wengi wao wakiwa maafisa wapya waliochaguliwa wa UDA, Dkt Ruto aliahidi kukamilisha miradi iliyokwama tangu enzi za Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kupanua ile iliyoanzishwa na utawala wake.

Alipuuza madai kwamba eneo hilo limetengwa kufuatia kung’olewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Rais alitangaza kuongezwa kwa ufadhili wa miundombinu muhimu, ikiwemo Sh4 bilioni kwa barabara za Mau Mau za urefu wa kilomita 700 na Sh 2 bilioni zaidi kwa mpango wa ziada wa kilomita 500 pamoja na Sh1 bilioni kwa uboreshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Nyeri.

Alieleza kuwa ushirikiano wake na ODM chini ya Serikali Jumuishi ni mradi wa kitaifa wa kuunganisha nchi, akiwataka wapigakura wa Mlima Kenya kukataa kurejea kwa siasa za kikabila.

Kisiasa, Rais anapiga vita madai ya usaliti na kudorora kwa maendeleo yanayotolewa na Bw Gachagua kwa kuonyesha miradi inayoonekana, mageuzi ya kiuchumi na kuimarisha upya mtandao wa UDA mashinani ili kudhibiti kupungua kwa uungwaji mkono katika Mlima Kenya.

Mkakati huo pia unahusisha kumtumia Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kuonyesha angali maarufu ilivyodhihirika katika ushindi wa UDA katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Mbeere North.

Rais aliwaambia viongozi hao kuwa madai ya kutengwa kwa Mlima Kenya hayana msingi, akisisitiza kuwa kila sehemu ya nchi itapata mgao wake wa rasilmali.

“Tumebuni mkakati wa kuwa na keki kubwa ya taifa itakayowanufaisha Wakenya wote,” alisema.

Alikumbusha uhusiano wake wa muda mrefu na eneo hilo tangu alipokuwa Waziri wa Kilimo wakati wa utawala wa marehemu Rais Mwai Kibaki hadi alipohudumu kama Naibu Rais wa Uhuru Kenyatta.

“Nimekuwa nikifanya kazi na watu wa mlima huu kwa zaidi ya miaka 20, sitawaacha kwa sababu ya kelele zisizo na maana,” alisema.

Rais alitetea Ushuru wa Nyumba akisema miradi hiyo tayari inaleta mabadiliko, huku vijana zaidi ya 500,000 wakipata ajira na nyumba 240,000 zikikamilishwa.

Pia alieleza kuwa mageuzi ya NSSF yameongeza akiba kutoka Sh 312 bilioni mwaka 2023 hadi 670 bilioni ndani ya miaka miwili, akisema ifikapo 2027 akiba itazidi Sh1 trilioni.

Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi alisema mkutano huo ulikuwa wa kuendeleza ziara ya Rais kaunti ya Nyeri wiki iliyopita, akisema mapokezi aliyopata yanaashiria kurejea kwa uungwaji mkono.

Hata hivyo, upinzani umepuuza juhudi hizo, ukisema wakazi wa Mlima Kenya tayari wameamua.

Mbunge wa Mukurweini John Kaguchia na mwenyekiti wa DEP Titus Ntuchiu walisema utawala wa Kenya Kwanza umeshindwa kutimiza ahadi zake, wakisisitiza kuwa Wakenya wanatafuta uongozi mbadala utakaoleta afueni dhidi ya gharama ya juu ya maisha na mzigo wa ushuru.