Trump aapa kuzidisha ada kwa nchi za Uropa zinazompinga kuchukua Greenland
WASHINGTON, AMERIKA
RAIS Donald Trump mnamo Jumamosi aliapa kutekeleza msururu wa ada kwa wandani Uropa hadi Amerika itakapoipata Greenland, jambo linalozidisha mgogoro kuhusu hatima ya kisiwa hicho kikubwa cha Denmark.
Kupitia ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema ushuru wa ziada wa asilimia 10 utaanza kutozwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Denmark, Norway, Sweden, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Finland na Uingereza, kuanzia Februari 1.
Ada hizo za ushuru zitaongezeka hadi asilimia 25 mnamo Juni 1 na zitaendelea hadi mkataba utakapofanikishwa kuruhusu Amerika kununua Greenland, aliandika Trump.
Trump amesisitiza mara kadhaa kuwa hatokubali chochote chini ya kumiliki Greenland, eneo linalojitawala la Denmark.
Viongozi wa Denmark na Greenland wamesisitiza kisiwa hicho si cha kuuzwa na hawataki kuwa sehemu ya Amerika.
Kura ya maoni iliyoendeshwa na Reuters/Ipsos wiki iliyopita ilibaini kuwa chini ya moja miongoni mwa wahojiwa watano wanaunga mkono wazo la kutwaa Greenland.
Rais amesema mara kwa mara kuwa Greenland ni muhimu kwa usalama wa Amerika kwa sababu ya eneo lake na madini chungunzima, na hajakanusha kutumia mabavu kuitwaa.
Nchi hizi, zinazocheza mchezo hatari mno, zimeweka kiwango cha tishio katika mchezo usioweza kustawishwa,” aliandika Trump.
Waandamanaji nchini Denmark na Greenland waliandamana Jumamosi kupinga matakwa ya Trump na kuitisha eneo hilo kuachwa kuamua hatima yake binafsi.
Mataifa yaliyotajwa na Trump Jumamosi yaliunga mkono Denmark, yakionya hatua ya Amerika kutumia jeshi kutwaa eneo ambalo ni mwanachama wa NATO huenda ikasambaratisha muungano wa jeshi unaoongozwa na Washington.
Vitisho vya Jumamosi huenda vikalemaza mikataba aliyofanikisha Trump mwaka jana na Muungano wa Uropa na Uingereza.
Mikataba hii ilijumuisha kiwango cha chini zaidi cha asilimia 15 ya ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Uropa na asilimia 10 kwa sehemu kubwa ya bidhaa za Uingereza.