Mkenya afariki katika mlipuko wa gesi Amerika
MAJIRA ya alasiri Desemba 23, 2025, yaligeuka huzuni kuu kwa familia ya muuguzi Mkenya Felistas Muthoni Nduthu, 52, aliyekufa kwenye mlipuko mkubwa katika nyumba ya wazee ya Bristol Health & Rehab Center, Jimbo la Pennsylvania, Amerika.
Bi Nduthu, aliyekuwa akihudumu zamu yake ya mwisho kabla ya kusafiri kwenda North Carolina kuungana na familia yake kwa sherehe za Krismasi, alikuwa akiwasaidia wazee katika kituo hicho. kujiandaa kwa sikukuu.
Hiyo ndiyo wakati ambao wafanyakazi waliporipoti harufu ya gesi. Ilikuwa majira ya saa nane mchana.
Wahandisi wa kampuni ya nishati ya PECO walifika kukagua hali hiyo.Dakika chache baadaye, mlipuko mkubwa ulitikisa jengo hilo, ukifuatiwa na mlipuko wa pili wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.
Zaidi ya watu 20 walikimbizwa hospitalini wakiwa na majeraha.
Wanawake wawili walipoteza maisha yao mmoja akiwa mkazi wa kituo hicho na mwingine akiwa Nduthu, mhudumu wa afya aliyejitolea, Mkatoliki mwenye imani thabiti na ambaye ni mama wa watoto watatu: Clinton (30), Joseph (24) na K.K. (18).
Wenzake kazini wanamkumbuka kama “taa ya matumaini” ambaye uwepo wake uliwatuliza wagonjwa.
“Alifanya kazi yake kama huduma, si ajira,” alisema mmoja wao.
Familia yake nchini ilipokea habari hizo kwa mshtuko. Dada yake, Petronilla Wanjugu Nduthu, aliandika, “Kabla ya Desemba 24 kuanza, nilipokea habari kuwa dada yangu ameaga dunia. Krismasi hii mioyo yetu imevunjika.”
Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mlipuko huo, huku uvujaji wa gesi ukiwa miongoni mwa sababu zinazochunguzwa.
Muungano wa wauguzi Amerika unataka haki kuhusu mauti yake kwa kushirikiana na familia.
Bi Nduthu pia alikuwa dadake marehemu Karimi Nduthu, mtetezi wa haki za binadamu aliyeuawa na utawala wa Moi mwaka 1996 kumbukumbu ya familia iliyolipa gharama kubwa kwa huduma na haki