Kimataifa

Uganda yarejesha huduma za intaneti, isipokuwa mitandao ya kijamii

Na REUTERS January 20th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KAMPALA, Uganda

SERIKALI ya Uganda imerejesha japo kwa kiwango fulani tu, huduma za mawasiliano baada ya Rais Yoweri Museveni kutangazwa mshindi katika uchaguzi mkuu, ushindi ambao umepingwa na upinzani.

Kutokana na ushindi huo uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Jumamosi, Museveni, 81, sasa alipata kibali cha kuongoza Uganda kwa muhula wa saba utakaomwezesha kuwa mamlakani kwa karibu miongo mitano.

Mnamo Jumapili asubuhi, baadhi ya watumiaji walisema waliweza kuwasiliana kwa njia ya intaneti. Vile vile, baadhi ya kampuni za kutoa huduma za intaneti zilituma jumbe kwa wateja zikisema kuwa mamlaka ya mawasiliano nchini Uganda iliziamuru kurejesha huduma, isipokuwa zile za mitandao ya kijamii.

“Tumerejesha mawasiliano kwa njia ya intaneti ili biashara zinazotegemea intaneti zirejelee shughuli,” David Birungi, msemji wa kampuni ya Airtel Uganda, mojawapo ya kampuni kubwa za mawasiliano nchini humo, aliambia shirika la habari la Reuters.

Aliongeza kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Uganda (UCC) iliamuru kuwa mitandao ya kijamii isalie kuzimwa.

Mamlaka hiyo ilisema ilizima mawasiliano ya intaneti kuzuia usambazaji wa “habari za kupotosha, habari zisizo sahihi, visa ya udanganyifu uchaguzini na aina zingine za madhara.”

Hata hivyo, upinzani ulikosoa hatua hiyo ukisema ililenga kuhakikisha kuwa serikali inadhibiti mchakato wa uchaguzi na kumhakikishia Rais Museveni ushindi.

Msemaji wa mamlaka ya UCC Ibrahim Bbosa hakujibu ombi la Reuters la kuzungumzia suala hilo.

Mnamo Jumamosi wiki jana Tume ya Uchaguzi nchini Uganda ilimtangaza Museveni mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi wiki hiyo kwa kuzoa asilimia 71.6 ya kura huku mpinzani wake mkuu Bobi Wine akipata asilimia 24 ya kura zilizopigwa na kuhesabiwa.

Ripoti moja iliyotolewa na kundi la waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika (AU), na jumuia zingine za kikanda, zilikosoa kuhusishwa kwa wanajeshi katika uchaguzi.

Aidha, makundi hayo yalikerwa na hatua ya serikali ya Uganda kuzima mawasiliano ya intaneti.

“Kuzimwa kwa intaneti kulikofanywa siku mbili kabla ya uchaguzi kulilemaza upatikanaji wa habari, uhuru wa kutangamana na kukwamiza shughuli za kiuchumi. Hatua hiyo pia iliibua mazingira ya shauku na kutoamini mchakato wa uchaguzi,” kundi la waangalizi wa AU lilisema katika ripoti yake iliyochapishwa Jumamosi.

Rais Museveni amedumu mamlakani tangu 1986 na wakati huu ni rais wa tatu Afrika kuhudumu kwa miaka mingi zaidi.

Kwa kupata nafasi ya kuongoza kwa muhula mwingine wa miaka mitano, ina maana kuwa atakuwa ameongoza kwa karibu nusu karne muhula huu utakapokamilika mwaka wa 2031.

Inaaminika kuwa rais huyo anamwandaa mwanawe, Muhoozi Kainerugaba, kurithi mamlaka kutoka kwake.

Kaineruga, ambaye wakati huu ni mkuu wa majeshi ya Uganda, amewahi kuelezea nia ya kuwa rais.


Bobi Wine, ambaye alikuwa akikabiliana na Museveni katika kinyang’anyiro cha urais, kwa mara ya pili, amepinga matokeo ya uchaguzi wa urais akidai ulisheheni visa kadha vya udanganyifu.

Wafuasi wa upinzani walifanya maandamano hafifu Jumamosi jioni baada ya matokeo ya uchaguzi wa urais kutangazwa, kulingana na wanahabari wa Reuters na polisi.