• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Istilahi muhimu katika taaluma ya Isimu

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Istilahi muhimu katika taaluma ya Isimu

Na MARY WANGARI

KUNA istilahi kadha ambazo ni muhimu katika taaluma ya Isimu.

Utendaji

Ni kile anachosema  mjua lugha katika muktadha wa mawasiliano ikiwa ni pamoja na makosa ya kiutendaji ya bahati mbaya na yale ya kukusudiwa. Vile vile tunaweza kusema ni udhihirikaji wa ujuzi wa lugha alionao mjua lugha.

Utumizi  (functionalism) na Urasmi (formalism)

Utumizi au isimu tumizi ni elimu inayohusu muundo wa lugha kwa kurejelea kazi zake za kijamii katika mawasiliano. Inamchukulia mtu binafsi kama kiumbe jamii na kuchunguza namna anavyojifunza lugha na kuitumia katika mawasiliano na wanajamii wenzake.

Urasmi au isimurasmi ni elimu ya maumbo dhahania ya lugha na mahusiano yake ya ndani.

Huzingatia maumbo ya lugha kama uthibitisho wa kimalimwengu bila kuzingatia namna jamii inavyowasiliana.

Uelezi na Uelekezi

Uelezi (isimu elezi) – ni mtazamo ambao huelezea ukweli wa lugha jinsi ilivyo na inavyotumika na jamiilugha husika. Na siyo namna inavyotakiwa kutumika. Isimu elezi haiweki kanuni ngumu au sheria ngumu zozote zinazotokana na mawazo ya mtu juu ya lugha fulani bali huelezea lughakwa kuangalia namna lugha hiyo inavyojidhihirisha yenyewe.

Huelezea sheria na kanuni ambazo mzungumzaji mzawa ameziweka kichwani na zinazoakisi uwezo wake wa lugha. Kwa kifupi, haielezi wala kuagiza namna mtu anavyotakiwa kutumia lugha bali namna lugha ilivyo na inavyotumika na wamilisi wa lugha hiyo.

Uelekezi (isimu elekezi) – ni mtazamo unaojaribu kuweka kanuni za usahihi wa namna watu wanavyotakiwa kutumia lugha.

Fonetiki

Tawi hili huchunguza sauti zinazotamkwa na binadamu bila kuzingatia lugha yoyote.

Fonolojia

Hili ni tawi la sayansi ya isimu linaloshughulikia uchunguzi wa mfumo wa sauti katika lugha fulani mathalan uainishaji wa   irabu na konsonanti. Fonolojia hutumika kuunda alfabeti katika lugha fulani. Aghalabu kila lugha hutumia mfumo fulani wa sauti mahususi katika lugha hiyo pekee.

Mofolojia na Sarufi Maumbo

Hili ni tawi la isimu linalochunguza maneno ya lugha fulani, aina za maneno katika lugha, hasa upangaji wa mofimu mbalimbali zitumikazo kwa ajili ya kuunda maneno hayo.

Kwa mfano, lugha ya Kiswahili hutumia mbinu kadha kuunda maneno kulingana na mpangilio wa mofimu.

Kwa mfano, neno ‘lima’ linaweza kutumika kuunda maneno mengine katika Kiswahili mathalan mkulima, kilimo, nimelima, limika na kadhalika. Katika kubadilisha mofimu hizi, tunaweza kubadilisha neno moja kutoka aina moja (kitenzi) hadi nyingine (nomino) na kadhalika.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Todd, L., (1987). An Introduction to Linguistics. Essex: Longman Group Limited.

TUKI (1990).  Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha. Dar es Salaam: Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Yule, G. (2010). The Study of Language (4th ed.). Cambridge: Cambridge University Press.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Uhusiano wa Isimujamii na...

FUNGUKA: ‘Nimeingiza wanne boksi’

adminleo