Wazazi washirikiane kuwafunza wanao uwajibikaji
BAADHI ya wazazi husubiri hadi watoto wao wakomae ndipo waanze kuwafunza kuhusu uwajibikaji.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya malezi na maendeleo ya watoto wanasema kuwa ni kosa kubwa kufanya hivyo, kwani misingi ya maadili na tabia njema hujengwa mapema – yaani kuanzia utotoni.
Katika familia nyingi za Kiafrika, watoto hufundishwa kuwa watiifu, lakini si mara zote hufundishwa kuhusu kuwajibika. Kwa mfano, mtoto anaweza kuamrishwa kusafisha chumba, lakini haelewi kwa nini kufanya hivyo ni muhimu kwake binafsi au kwa familia kwa jumla.
“Mtoto akifundishwa kuosha kikombe chake mwenyewe baada ya kutumia, au kupangusa meza baada ya kula, anaanza kuelewa kuwa kila tendo lina athari na kila mtu ana jukumu fulani katika familia,” asema Bi Loice Okello, mtaalamu wa masuala ya malezi na ushauri wa familia.
Wanandoa wanapaswa kukubaliana kuhusu mbinu ya pamoja ya kuwalea watoto wao ili kuhakikisha msimamo wa pamoja katika malezi.
Hili linasaidia kuepusha mkanganyiko ambapo mzazi mmoja anasisitiza nidhamu na uwajibikaji, huku mwingine akimpendelea mtoto kwa kisingizio cha kwamba ‘bado ni mdogo’.
Wataalamu wanashauri kuwa watoto kuanzia umri wa miaka miwili wanaweza kuanza kufunzwa uwajibikaji kupitia michezo, mazungumzo ya kila siku, na hata kuiga yale wazazi wao wanafanya.
“Lazima umfundishe mtoto uwajibikaji akiwa na umri mdogo. Usisubiri hadi akomae au afike shule ya upili ndipo uanze kumweleza maana ya majukumu. Malezi hujengwa hatua kwa hatua,” anasisitiza Bi Okello.
Kufunza uwajibikaji mapema hujenga misingi ya nidhamu, heshima na uwezo wa mtoto kufanya maamuzi mazuri maishani.
Mtoto anayejua majukumu yake akiwa mchanga hujisimamia kimaisha bila tatizo na kutekeleza wajibu wake hata anapoanza shule au anapokuwa mtu mzima.
Wazazi wasisubiri mtoto apate matatizo au ashindwe maishani ndipo waanze kumlaumu au kulaumu mfumo wa elimu. Jukumu la malezi bora huanzia nyumbani, na ni la pamoja kwa mama na baba bila kumwachia mzazi mmoja pekee.
Kwa hivyo, wazazi wote—iwe wanaishi mjini au vijijini—wanapaswa kuelewa kuwa mtoto hufunzwa si kwa maneno matupu, bali kwa matendo ya kila siku. Kumpa mtoto jukumu dogo kama kupanga viatu, kusaidia kupika au kufagia si kumtesa, bali ni kumwandaa kuwa raia mwema, mwenye bidii na anayejitegemea maishani.