Kimataifa

Besigye alemewa jela, akimbizwa hospitalini akiwa ‘hali mahututi’

Na DAILY MONITOR January 21st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa upinzani Uganda Dkt Kizza Besigye aliondolewa gerezani na kukimbizwa hospitali baada ya afya yake kudorora na kufikia hali hatari usiku wa kuamkia Jumanne.

Besigye, kiongozi wa PFF amekuwa gerezani kwa muda sasa na alipokuwa akikimbizwa hospitalini, msafara wake uliandamana na maafisa wengi wa usalama.

“PF ingependa kuwaarifu wafuasi wake na umma kuwa afya ya Dkt Kizza Besigye imedorora na kufikia hali hatari,” ikasema taarifa ya chama iliyotundikwa katika mtandao wa X saa nane na dakika 31 usiku wa kuamkia Jumanne.

PFF ilisema ilipokea habari kuwa Dkt Besigye alihamishwa kutoka gereza la Luzira hadi hospitali moja jijini Kampala.

“Alikimbizwa hospitalini chini ya ulinzi mkali hadi hospitali inayopatikana Bugolobi, Kampala,”  ikaongeza

Chama hicho kilishutumu serikali kwa kumnyima Besigye huduma bora za kimatibabu na kuendelea kuzuiliwa kwake ni kumnyima haki zake za kimsingi.

“Ni janga kuwa mwanaume ambaye alipigania uhuru na afya kwa wengine sasa ananyimwa haki ya kupokea matibabu. Chochote kikimfanyikia, serikali na gereza ndizo zitawajibika,”  ikasema taarifa hiyo.

PFF pia ilitoa amri kuwa madaktari wa kibinafsi wa Besigye na wanafamilia wake waruhusiwe  kumwona bila kuzuiwa na ikasema anaendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria.

“Lazima awaachiliwe ili  apate matibabu anayostahili,” PFF ikasema na kuwataka wafuasi wake wakae ange na pia kumwombea Besigye.

Daily Monitor haikuweza kuthibitisha madai hayo kwa sababu wakati wa kuchapisha habari hizi Jumanne usimamizi wa magereza haukuwa umejibu simu au jumbe walizotumiwa.

Besigye alikuwa daktari wa kibinafsi wa Rais Yoweri Museveni na amekuwa mpinzani wake mkuu katika chaguzi nne.

Amekuwa akizuiliwa kwa siku zaidi ya siku 350 tangu arejeshwe Uganda kutoka Nairobi. Kortini anapambana na mashtaka yanayohusishwa na ugaidi na hajawahi kuachiliwa kwa dhamana.

Mara ya mwisho alipokuwa mahakamani ni Disemba 30, 2025 ambapo pamoja na Obed Lutale na Kapteni Denis Oola, walikanusha mashtaka dhidi yao baada ya awali kukataa kufanya hivyo kwenye Mahakama Kuu ya Kampala.

Jaji Emmanuel Baguma aliratibisha Januari 21 (leo) kama siku ambao Besigye na wenzake wanastahili kufika kortini.

Awali mwaka jana, iliripotiwa Besigye alikuwa mgonjwa sana baada ya kususia kula gerezani akisaka haki.

“Huko ni kuhadaa na kuvutia huruma kutoka kwa umma. Huwezi kushtakiwa kwa makosa mazito kisha unatumia kususia chakula kama mbinu ya kusaka huruma ndipo uwaachiliwe kwa dhamana,”  akasema Rais Museveni akizungumzia masaibu ya Besigye.

“Mbona unataka mashtaka dhidi yako yaharakishwe?

Museveni alisisitiza kuwa kuna hospitali ya serikali ndani ya gereza kushughulikia matibabu ya Besigye pamoja na mahabusu wengine.