Kimataifa

Upinzani Uganda bado haupumui naibu wa Bobi Wine akikamatwa

Na REUTERS January 23rd, 2026 Kusoma ni dakika: 1

KAMPALA, UGANDA

UPINZANI nchini Uganda hauonekani kupumua baada ya polisi jana kuthibitisha kuwa wanamzuilia mbunge ambaye pia ni afisa wa ngazi ya juu wa chama kikuu cha upinzani NUP.

Polisi wanasema mwanasiasa huyo anazuiliwa kutokana na ghasia ambazo zilitokea baada ya uchaguzi ambapo zaidi ya watu saba waliuawa.

Mbunge Muwanga Kivumbi ambaye pia ni makamu kiongozi wa NUP anazuiliwa kutokana na ghasia hizo.

NUP inaongozwa na Bobi Wine ambaye yuko mafichoni tangu wiki jana baada ya kubwagwa na Rais Yoweri Museveni kwenye uchaguzi uliofanyika mnamo Januari 15.

Polisi walithibitisha kupitia X kuwa Kivumbi anaendelea kuzuiliwa na angefikishwa mahakamani wakati wowote.

“Kukamatwa kwake kunahusiana na matukio ya ghasia za kisiasa baada ya uchaguzi,” polisi wakisema.

Hata hivyo, polisi na Kivumbi wametoa taarifa zinazokinzana kuhusu makabiliano kati ya wafuasi wa mbunge huyo na maafisa wa usalama mnamo Januari 15.

Polisi wanasema genge lililokuwa limebeba silaha kama vile panga na kupangwa na Kivumbi walivamia kituo cha polisi na kituo cha kujumuisha kura.

Kivumbi naye alisema watu waliuawa nyumbani kwake ambako walikuwa wakisubiri matokeo ya ubunge yatangazwe.

Alidai kuwa watu 10 waliuawa na kurejelea mauaji hayo kama ya ‘halaiki’.

Katibu Mkuu wa NUP David Rubongoya alisema bado wanasaka ufafanuzi zaidi kuhusu kukamatwa kwa Kivumbi kabla ya kutoa taarifa.

Mamia ya wafuasi wa NUP walikamatwa wakati wa kampeni na baada ya uchaguzi huku uongozi wa chama hicho ukisema ilikuwa njia ya kuwaingiza uoga.

Wine ambaye yuko machifoni, alidai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu na akatoa wito kwa Umoja wa Afrika uzungumzie mauaji na ukandamizaji wa haki unaoendelea Uganda.