Tuko tu sawa! ANC yakataa kufufuka, yakosoa uamuzi wa korti
CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimekosoa vikali uamuzi wa Mahakama Kuu uliotangaza kuwa muungano kati yake na Amani National Congress (ANC) kilichoongozwa wakati mmoja na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi haukuwa wa kikatiba, kikisema kuwa mahakama ilibatilisha muungano ambao haujawahi kuwepo kisheria.
Katika taarifa iliyotoa jana, UDA kupitia Naibu Kiongozi wa chama, Bw Issa Timamy, ilisema kuwa uamuzi uliotolewa Alhamisi, Januari 22, ulikuwa umepitwa na wakati, ikisisitiza kuwa ANC haikuungana na UDA bali ilijivunja yenyewe kwa hiari kwa kuzingatia Katiba yake na Sheria ya Vyama vya Kisiasa.
Taarifa hiyo ilitolewa kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na Jaji Bahati Mwamuye, ambaye aliamua kuwa kuvunjwa kwa ANC na madai ya kuunganishwa kwake na UDA hakukutimiza viwango vya kikatiba vinavyohitajika kuvunja au kuunganishwa vyama vya kisiasa, na hivyo ANC bado ni chama kilichosajiliwa kisheria.
Jaji Mwamuye pia alitangaza kuwa Notisi ya Gazeti la Serikali iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Kisiasa kurasmisha muungano huo ilikuwa kinyume cha sheria, batili na isiyo na nguvu ya kisheria, na akaagiza msajili huyo kurekebisha mara moja sajili rasmi ili kuonyesha kuwa ANC bado kipo kama chama kisheria.
Hata hivyo, UDA ilikataa tafsiri hiyo, ikirejelea Notisi ya Gazeti Na. 3449 ya Machi 14, 2025, ambapo aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Ann Nderitu ambaye kwa sasa ni Kamishna wa IEBC, alithibitisha kuwa ANC ilivunjwa baada ya Mkutano Maalum wa Wajumbe wa Kitaifa uliofanyika Februari 7, 2025.
Kwa mujibu wa UDA, uamuzi wa kuvunjwa kwa ANC ulikuwa wa hiari na ulifanywa na wanachama wa chama hicho kwa kuzingatia katiba ya chama na masharti husika ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa, hivyo basi hakukuwa na muungano wowote ambao ungeweza kutangazwa kuwa kinyume cha katiba na mahakama.
Chama hicho tawala kilisema kuwa kuwasilisha uamuzi wa mahakama kana kwamba umebatilisha muungano wa ANC na UDA ni upotoshaji wa ukweli, kikisisitiza kuwa mahakama haiwezi kubatilisha uamuzi ambao haujawahi kufanywa.
UDA ilisisitiza kuwa baada ya kuvunjwa kwa ANC, mali yote ya chama hicho ilihamishiwa kisheria kwa UDA, huku wanachama wa zamani wa ANC wakijumuishwa kikamilifu ndani ya chama tawala kupitia taratibu halali za kisheria na kiutawala.
Chama hicho pia kilipuuza madai kuwa uamuzi huo ungefufua kikisema kuwa hakukuwa na suitafahamu yoyote ya kisheria au kiutawala baada ya kuvunjwa kwa ANC.
“Kwa hivyo, kudai kuwa ‘muungano’ ulitangazwa kuwa ‘kinyume cha sheria’ na mahakama ni kubuni simulizi nyingine isiyo na msingi. Hauwezi kubatilisha uamuzi ambao haukuwahi kuwepo hata kidogo,” chama hicho kilisema.
ANC ilikubali kuingia ndani ya UDA kama sehemu ya juhudi za kuunda muungano mkubwa wa kisiasa, hatua iliyosababisha Rais William Ruto kubaki kuwa kiongozi wa chama, Naibu Rais, Kithure Kindiki akiteuliwa kuwa naibu kiongozi wa kwanza, huku nafasi mpya ya naibu kiongozi ikiundwa kushikiliwa na Gavana wa Lamu, Issa Timamy.
UDA ilisema kuwa itaendelea kulinda mshikamano wa chama, kuimarisha umoja wa ndani na kuunganisha wafuasi wake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, ambapo Rais Ruto analenga kutetea kiti chake.