Habari

Kimemramba! Mackenzie kushtakiwa kwa mauaji yaliyotokea katika Msitu wa Kwa Bi Nzaro

Na BRIAN OCHARO January 24th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MHUBIRI tata Paul Mackenzie anatarajiwa kushtakiwa kwa kosa la mauaji kuhusiana na wimbi la pili la vifo vinavyohusishwa na dhehebu haramu, katika Msitu wa Kwa Bi Nzaro, Kaunti ya Kilifi.

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) iliambia Mahakama ya Malindi Ijumaa kuwa imekamilisha kuchambua ushahidi na imeamua kumshtaki Mackenzie pamoja na washukiwa wengine sita wanaodaiwa kuendeleza ibada ya kufunga hadi kufa katika eneo la Kwa Bi Nzaro, kilomita chache kutoka eneo la awali la uhalifu ambako zaidi ya watu 450 walifariki.

“Tumechambua ushahidi na washukiwa wote watashtakiwa. Mmoja wa washukiwa tunayekusudia kumshtaki hayupo mahakamani leo, lakini tunatarajia kuwashtaki wote kwa pamoja. Hivi sasa anazuiliwa katika Gereza la Shimo La Tewa,” upande wa mashtaka uliambia mahakama.

Mkurugenzi wa Mashtaka alieleza kuwa Mackenzie hakuweza kuwasilishwa mahakamani kusomewa mashtaka kwa sababu amri ya kumfikisha mahakamani haikuwa imetolewa.

“Bila amri ya kumwasilisha, haingewezekana kumleta mahakamani leo. Tunahitaji Mackenzie na washukiwa wengine wote washtakiwe kwa pamoja,” upande wa mashtaka ulisema.

Serikali pia ilieleza mahakama kuwa inahitaji siku 14 kufanya maandalizi ya kumsafirisha Mackenzie hadi Malindi ili akabiliwe na mashtaka.

“Tunaomba amri ya kumwasilisha Mackenzie ili asomewe mashtaka pamoja na washukiwa wengine,” serikali iliongeza.

Mahakama pia iliambiwa kuwa Mackenzie amekuwa “akizungushwa kutoka mahakama moja hadi nyingine,” jambo lililofanya iwe vigumu kwa waendesha mashtaka kuomba amri ya kumwasilisha mapema.

“Washukiwa hawawezi kuachiliwa kwa dhamana. Wataendelea na kufunga na kueneza misimamo mikali,” upande wa mashtaka ulidai, ukiongeza kuwa ni busara kusoma mashtaka yote kwa wakati mmoja.

Kupitia wakili wao, washukiwa walisema hawapingi kutolewa kwa amri ya kumwasilisha Mackenzie, lakini walihoji kucheleweshwa kwa hatua hiyo na ODPP.

“Hatujapinga amri ya kumwasilisha. Hata hivyo, hatuelewi kwa nini ODPP haikuomba amri hiyo mapema,” upande wa utetezi ulisema.

Pia walipinga ombi la kuongeza muda wa siku 14, wakisema washukiwa hawana hatia na wanazuiliwa bila haki.

“Hawa ni watu wasio na hatia wanaozuiliwa bila sababu za msingi,” utetezi ulidai.

Mahakama inatarajiwa kutoa maamuzi zaidi Jumatatu kuhusu ombi la ODPP la kutaka siku 14 ili kumwasilisha Mackenzie katika Mahakama ya Malindi kusomewa mashtaka mapya.

Mackenzie atashtakiwa pamoja na mhubiri Sharleen Temba Anido, Kahindi Kazungu Garama, Thomas Mukonwe na James Kahindi Kazungu kuhusiana na vifo vya watu 52 huko Kwa Bi Nzaro.

Washukiwa wengine watatu ambao ni Julius Thuva, Charles Mutua na Johnson Gona pia wameongezwa katika kesi hiyo.