Wakongwe ndio kusema bungeni Uganda
UCHAGUZI wa wabunge nchini Uganda unakaribia kukamilika huku makundi maalum, yakiwemo watu wenye ulemavu, wazee, wafanyakazi na vijana yakichagua wawakilishi wao katika Bunge la Taifa.
Muhula wa Bunge la sasa unatarajiwa kumalizika Mei, baada ya hapo Bunge la 12 litaapishwa na kuanza kazi mara moja.
Bunge jipya litakapokutana, taswira moja itajitokeza wazi licha ya Uganda kuwa na idadi kubwa ya vijana: uwepo wa wabunge wenye umri wa zaidi ya miaka 80, ambao wameibuka washindi tena, sawa na Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, anayesisitiza kuwa bado ndiye nahodha bora wa kuongoza nchi hiyo.
Kuchaguliwa kwa viongozi hawa wazee kunaonekana kama kauli nzito kuhusu kudumisha uongozi, uaminifu na uthabiti sifa ambazo Waganda wengi wanaamini ndizo msingi wa maendeleo ya kiuchumi ya taifa hilo.
Jenerali Moses Ali, 87 mwanajeshi mkongwe alichaguliwa tena kuwa Mbunge wa Adjumani Magharibi akiwa na umri wa miaka 87. Safari yake ya kisiasa imepitia tawala tofauti, migogoro ya kijeshi na mabadiliko ya katiba.
Kwa wafuasi wake, ushindi wake ni ushahidi kuwa tajriba bado ina thamani, kuwa huduma ya muda mrefu hujenga imani, na kuwa uongozi unatokana na busara inayojengwa kwa miaka, si umri pekee.
Ali amekuwa karibu na mamlaka kwa zaidi ya nusu karne, akishikilia nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Waziri wa Fedha wakati wa utawala wa Rais wa zamani Idi Amin katika miaka ya 1970.
Ali alizaliwa Oktoba 1939 huko Adjumani, kaskazini mwa Uganda karibu na mpaka wa Sudan Kusini
Ni mmoja wa wanasiasa waliodumu kwa muda mrefu na wenye historia changamano nchini humo. Kuchaguliwa kwake kumezua mjadala kuhusu uwezo wake wa kuendelea kuwatumikia wakazi wa eneo lake ipasavyo.
Alijipatia umaarufu wa kitaifa miaka ya 1970 lakini alitoroka nchi baada ya kuporomoka kwa utawala wa Amin. Baadaye aliongoza kundi la waasi la Uganda National Rescue Front (UNRF) katika eneo la West Nile mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Ali amehudumu katika nyadhifa za juu serikalini, ikiwemo Naibu Waziri Mkuu, huku akiendelea kuwakilisha Adjumani Magharibi bungeni mara kadhaa.
Profesa Ephraim Kamuntu, 81 aliyezaliwa Septemba 1945 ni msomi na mwanasiasa mkongwe mwenye tajriba ndefu katika masuala ya utawala na maendeleo ya kiuchumi.
Ni rafiki wa muda mrefu wa Rais Museveni tangu waliposoma pamoja katika Shule ya Ntare, Mbarara. Kamuntu alisomea uchumi katika Chuo Kikuu cha Makerere na baadaye kusomea usimamizi na utawala wa biashara katika Chuo Kikuu cha Massachusetts, Amerika. Amewahi kufundisha katika vyuo vikuu vya Makerere na Nairobi kabla ya kujiunga na siasa miaka ya 1980. Awali alikuwa upande wa upinzani, baadaye alijiunga na chama tawala na amekuwa mwakilishi wa Sheema Kusini magharibi mwa Uganda.
Ameshikilia nyadhifa mbalimbali za uwaziri na kuhudumu kama mshauri wa rais. Wachambuzi wanaamini anaweza kurejea Baraza la Mawaziri baada ya Museveni kuapishwa kwa muhula wake wa saba Mei.
Matia Kasaija, aliyezaliwa Mei 1944, ni mmoja wa mawaziri waliodumu kwa muda mrefu zaidi nchini Uganda. Amekuwa Waziri wa Fedha tangu 2015 na ni Mbunge wa Buyanja, Wilaya ya Kibaale.
Mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Ntare na mhitimu wa biashara kutoka Makerere, Kasaija alijiunga na siasa za uchaguzi mwaka 1980 na kushinda kiti cha ubunge. Aliwahi kuteuliwa Waziri wa Nchi anayehusika na Kazi na Rais Milton Obote, kabla ya kujiunga na waasi wa Museveni waliotwaa mamlaka mwaka 1986.
Kasaija amehudumu pia katika bodi za taasisi mbalimbali za kimataifa zikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, IMF, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu. Akiwa Waziri wa Fedha, amesimamia ukuaji wa uchumi lakini pia amekosolewa kwa sera zinazodaiwa kuwa mzigo kwa vijana. Deni la Uganda limepanda hadi zaidi ya asilimia 50 ya Pato la Taifa chini ya uongozi wake. Wabunge wengine kadhaa watatimiza miaka 80 wakati wa muhula huu, wakiwemo wanajeshi waliopigana pamoja na Museveni msituni kama Jenerali Kahinda Otafiire (Masuala ya Ndani) na Jenerali Jim Muhwezi (Usalama).
Ingawa umri si tatizo kwa baadhi, vijana wengi wa Uganda wana wasiwasi kuwa viongozi wazee huweka mbele maslahi yao binafsi badala ya kufungua fursa kwa kizazi kipya. Kwa mfano, vijana wanaofanya kazi za kidijitali waliathirika pakubwa serikali ilipofunga mtandao na huduma za pesa kwa simu.
Wanasiasa vijana hukumbana na vikwazo vingi kama ukosefu wa fedha za kampeni, miundo migumu ya vyama na kushikiwa na wapiga kura kuhusu uwezo wao wa kuongoza. Huku wazee wa zaidi ya miaka 80 wakitawala siasa za uchaguzi, vijana wanauliza: ni lini, na kwa njia gani, watapokezwa kijiti cha uongozi?