Ruto amteua Ida Odinga Balozi wa Kenya katika UNEP
Rais William Ruto amemteua Ida Betty Odinga, mjane wa aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga, kuwa Balozi wa Kenya na Mwakilishi wa Kudumu katika Shirika la Umoja wa Mataifa kuhudu Mazingira (UNEP).
Katika taarika, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei, alisema uteuzi huo unatambua huduma ya Ida Odinga kwa umma. Koskei alieleza kuwa kazi yake ni ushahidi wa uongozi wa kujitolea, ujasiri, na dhamira ya kudumu ya kuendeleza elimu na uwezeshaji wa wanawake.
‘ Rais kwa kutumia mamlaka yake kama Kiongozi wa Nchi na Serikali, amemteua Dkt Ida Betty Odinga, E.G.H., kuwa Balozi/Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusy Mazingira (UNEP),’ ilisema sehemu ya taarifa ya Bw Koskei.
Taarifa hiyo pia ilitambua kazi ya utetezi ya Ida Odinga, ikitaja demokrasia, kukuza uhuru wa maoni, kuendeleza usawa wa kijinsia, na kushirikisha elimu kama msingi wa maendeleo ya taifa jumuishi.
Koskei alisema jina la Ida limewasilishwa kwa Bunge la Kitaifa kuzingatiwa na kuidhinishwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za Katiba zinazohusu uteuzi wa mabalozi.
Uteuzi huu unafuata mabadiliko ambayo aliyekuwa balozi WA Kenya katika UNEP, Ababu Namwamba, alihamishiwa Uganda. Namwamba alichukua nafasi ya Joash Maangi, ambaye alihamishiwa Brussels, Ubelgiji, kuwakilisha Kenya katika Tume ya Ulaya.