Habari

Uamuzi wa Trump kujiondoa katika shirika la WHO kugonga Kenya

Na HELLEN SHIKANDA January 24th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya miaka 78 kama mwanachama mwanzilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Amerika imejiondoa rasmi katika shirika hilo la kimataifa la afya, uamuzi ambao utaathiri mataifa mengi ikiwemo Kenya.

Katika taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari, Waziri wa Masuala ya Nje, Marco Rubio na Waziri wa Afya na Huduma za Kibinadamu Robert F. Kennedy Jr walisema Amerika iliamua kujiondoa kufuatia kile walichotaja kama kushindwa kwa WHO wakati wa janga la Covid-19.

“Kuanzia sasa, ushirikiano wa Amerika na WHO utakuwa tu katika kutekeleza hatua za kujiondoa na kulinda afya na usalama wa raia wa Amerika.

Ufadhili wote wa Amerika kwa WHO na ushiriki wa wafanyakazi wake katika mipango ya shirika hilo umesitishwa,” ilisema taarifa hiyo.

Waliongeza kuwa Amerika itaendelea kuongoza dunia katika masuala ya afya ya umma kwa kuokoa maisha ya mamilioni ya watu na kuwalinda raia wake kwa kuzuia magonjwa ya kuambukiza kufika nchini humo, huku ikiendeleza usalama wa afya ya kimataifa kupitia ushirikiano wa moja kwa moja baina ya mataifa.

Kwa mujibu wa WHO, Amerika ilichangia takriban Sh165.5 bilioni katika kipindi cha miaka miwili cha 2022–2023.

Fedha hizo ziliwezesha WHO, Amerika na mataifa mengine kutambua na kukabiliana na dharura za kiafya, kuzuia kuenea kwa magonjwa kuvuka mipaka, na kuendeleza vipaumbele muhimu vya afya ulimwenguni.

Lakini hatua hiyo ina maana gani kwa Kenya?

Dkt Patrick Amoth, Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya katika Wizara ya Afya, aliambia Taifa Dijitali kuwa, kujiondoa kwa Amerika ni pigo kubwa kwa WHO kwani ilikuwa mfadhili wake mkubwa zaidi. Alieleza kuwa ingawa hatua hiyo imetekelezwa mwaka huu, WHO ilikuwa tayari imeanza kujiandaa tangu baada ya janga la Covid-19.

“Ni pigo, lakini WHO imeanza kuchukua hatua za kupunguza athari kwa kuhakikisha nchi wanachama zinaongeza taratibu michango yao ya lazima,” alisema.

WHO ina wanachama 174, idadi ambayo itapungua hadi nchi 173, na iwapo nchi hizo zitatekeleza wajibu wao wa kifedha kikamilifu, pengo hilo linaweza kuzibwa.

Dkt Amoth alisema ana wasiwasi kuwa baadhi ya mipango inaweza kuathirika, lakini anaamini athari zake kwa Kenya na hata kwa WHO kwa ujumla zitakuwa chache zaidi ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka minne au mitano iliyopita.

Aliongeza kuwa washirika wengine wa maendeleo wanaounga mkono mifumo ya afya, hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati, watakuwa na mchango mkubwa katika kuziba pengo hilo.

Nchini Kenya, WHO imekuwa ikisaidia Wizara ya Afya katika mipango mbalimbali, ikiwemo afya ya uzazi, mama, watoto wachanga; maendeleo ya bidhaa na teknolojia muhimu za afya; pamoja na mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

“Msaada wao umekuwa mkubwa sana,” alisema Dkt Amoth.

Alikiri kuwa baadhi ya mipango inaweza kuathirika, lakini akasema wizara inasubiri mawasiliano rasmi kutoka WHO.“Baada ya hapo, tutaweka mikakati ya kuhakikisha mipango inaendelea,” alisema.

Alishauri Kenya na mataifa mengine kuwekeza zaidi katika huduma za afya ya msingi (PHC), kinga na uhamasishaji raia kuhusu afya, akisisitiza kuwa huduma hizo ni jumuishi na huleta manufaa makubwa kuliko kuwekeza zaidi katika huduma za tiba pekee.