Dhahabu nyeupe ya kilimo: Ufufuaji wa pareto
KENYA inaendelea kupiga hatua katika mikakati kufufua mojawapo ya mazao yake ya kibiashara yaliyowahi kuwa yenye thamani lakini yakaporomoka — pareto.
Miaka ya zamani, likijulikana kama “dhahabu nyeupe”, zao hili lilikuwa chanzo kikuu cha mapato ya kigeni na lilikuwa likisaidia zaidi ya wakulima 100,000 wenye mashamba madogo kabla ya kuanguka mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Sasa, kupitia juhudi za serikali, ubunifu wa kiteknolojia na ushirikiano wa sekta za binafsi, pareto inaanza kurejea katika nafasi yake kwenye kilimo cha Kenya.

Hata hivyo, zao hilo bado linalimwa kwa kiwango kidogo kwa karibu kaunti 19. Aghalabu, wakulima wengi ni wanaozalisha kwenye nusu ekari na ekari moja.
Kwenye Kongamano la Kitaifa la Kilimo-Biashara 2025, lililoandaliwa na Agriculture Sector Network (ASNET) kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo na Mifugo, wadau walisisitiza umuhimu wa mifumo ya kidijitali, kukumbatia bunifu za teknolojia kufufua na kuboresha sekta ya pareto nchini.
Kongamano hilo lenye kaulimbiu “From Promise to Action: Advancing Agribusiness through Dialogue and Innovation”, liliandaliwa Jijini Nairobi mnamo Oktoba 22 na 23.

Afisa Mkuu Mtendaji wa ASNET, Agatha Thuo, alisema ukuaji wa pareto utachochewa zaidi na mifumo ya teknolojia za kisasa.
“Mazao yaliyosahaulika kama pareto yanaweza kufufuliwa kupitia mbinu za kisasa na wakulima wanapaswa kuachana na mbinu za zamani ili kuwa bora kikanda na kimataifa kwenye uzalishaji,” Agatha alielezea.
Serikali imekuwa ikipunguza gharama za uzalishaji katika kilimo kupitia mbolea ya ruzuku, upimaji wa udongo na uhamasishaji wa matumizi ya bunifu za kiteknolojia.

Kongamano la ASNET liliwaleta pamoja viongozi wa kitaifa, sekta ya binafsi, washirika wa kilimo wakiwemo watafiti na vikundi vya wakulima kujadili njia faafu kubadilisha mifumo ya kilimo Kenya, ili kiwe sekta endelevu na yenye ushindani mkuu.
Lilikuwa na maonyesho, na miongoni mwa walioshiriki, kilikuwa kiwanda cha kiserikali cha pareto nchini, ndicho Pyrethrum Processing Company of Kenya (PPCK).
Collins Omondi, mtafiti PPCK, alisema kampuni hiyo inalenga kuzalisha mbegu bora, kuchakata maua ya pareto na kuongeza thamani kupitia utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za zao hilo.

Bidhaa zake ni pamoja na Pyagro — dawa ya kuua wadudu kwenye mboga na matunda, na Pareto Roach Spray – ya mende na kunguni. Pia, kuna Paresol, dawa dhidi ya mbu. “Bidhaa hizi zimefungua ajira nyingi katika kila mtandao wa uongezaji thamani,” Omondi alisema.
Pareto inathaminiwa kimataifa kwa kuwa salama kwa mazingira na kutokuwa na sumu kwa binadamu na mifugo.
Kwa sasa, nchini karibu wakulima 5,000 wanajihusisha na ukuzaji wa zao hili, ikilinganishwa na zaidi ya 100,000 miaka ya 1980.

Takwimu kutoka Wizara ya Kilimo zinaonyesha Kenya inazalisha karibu tani 300 za maua ya pareto kila mwaka, nusu ya kiwango hicho ikitumika nchini na nyingine kuuzwa Ulaya, Amerika na Asia.
Kuporomoka kwa sekta ya pareto kulisababishwa na malipo duni na yaliyokuwa yakicheleweshwa kwa wakulima, dawa bandia za bei nafuu na kanuni kali katika masoko ya kimataifa.

Hata hivyo, Omondi kwenye mahojiano na Akilimali alidokeza kwamba mageuzi yanayoendelea yatarejesha matumaini. PPCK inalenga kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari 10,000 hadi 70,000 na kuhamasisha vijana kushiriki.
Ni sekta ambayo kulingana na Omondi, ikipigwa jeki itasaidia kutatua suala la ukosefu wa ajira nchini haswa miongoni mwa vijana.
