Kimataifa

Video zaanika mauaji yalivyotokea Minnesota utawala wa Trump ukijitetea

Na REUTERS January 27th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MINNEAPOLIS, Amerika

MAAFISA wa serikali ya Rais wa Amerika Donald Trump wametetea kisa cha Jumapili ambapo maafisa wa idara ya uhamiaji walimuua kwa kumpiga risasi raia mmoja, huku uhasama ukipanda kati ya viongozi wa Democrat na maafisa wa serikali hiyo.

Maafisa wa Trump walieleza kuwa raia huyo Alex Pretti, aliwashambulia maafisa hao wa Idara ya Uhamiaji na ndipo wakamfyatulia risasi kama hatua ya kujikinga.

Lakini maelezo hayo yalikinzana na video zilizonaswa na watu waliokuwa katika eneo la tukio, zilizoonyesha kuwa Pretti hakuanzisha ugomvi na maafisa hao.

Pretti ni Mwamerika wa pili kuuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa uhamiaji mwezi huu katika mji wa Minneapolis, ambako Trump amewatuma maelfu wa maafisa wenye silaha kufanikisha operesheni ya kuwafurusha wahamiaji.

Gavana wa Minnesota Tim Walz, wa chama wa Democrat, kwa mara nyingine alimtaka Trump kuondoa maajenti wa serikali yake kutoka jimbo hilo. Maafisa wa jimbo hilo wameitaka Mahakama kuharamisha operesheni hiyo inayoendeshwa na utawala wa Trump wakiitaja kama inayokiuka katiba.

“Waathiriwa ni maafisa wa kulinda doria mpakani,” Gregory Bovino, afisa wa cheo cha juu katika kitengo hicho cha kulinda doria mpakani akasema katika kipindi cha “State of the Union” kwenye shirika la habari la CNN.

Maelezo hayo, yaliyoungwa mkono na Waziri wa Usalama wa Ndani Kristi Noem na maafisa wengine wa utawala wa Trump, yaliibua hasira miongoni mwa viongozi wa chama cha Democrat na wabunge wa chama hicho cha upinzani.

Walirejelea video zilizonaswa na mashahidi zilizoonyesha kuwa kile ambacho Pretti alikuwa ameshikilia ni simu ya mkononi pekee, kabla ya maafisa hao kumvamia, kumwangusha na hatimaye kumpiga risasi kwa karibu.

Katika muda wa wiki kadhaa zilizopita, maafisa hao wa serikali ya Amerika wamekabiliwa na raia wenye hasira wakipinga operesheni yao, huku baadhi ya raia hao wakipiga firimbi.

Kwa mara nyingine maelfu ya watu walifurika katika barabara za jiji la Minneapolis Jumapili wakipinga operesheni inayoendeshwa na maafisa wa Idara ya Uhamiaji.

Video za mauaji ya Jumamosi zilizothibitishwa na Reuters, zilimwonyesha Pretti, 37, akishika simu mkononi, wala sio bunduki, huku akijaribu kuwasaidia waandamanaji wengine walioangushwa na maajenti wa Idara ya Uhamiaji.

Pretti anaonekana akinasa video kwa simu yake huku afisa mmoja wa utawala wa Trump akiwasukuma wanawake wawili na kuwaangusha.

Pretti anaonekana akiinua mkono wake wa kushoto kujikinga dhidi ya pilipili ya unga aliyonyunyiziwa na afisa mmoja wa serikali.

Kisha ghafla maafisa wengine wanamkamata Pretti na kumwangusha chini. Huku wakiwa wamemfinya chini, mmoja wao anasikika akionya kuhusu uwepo wa bunduki.

Kanda ya video inaonyesha afisa mmoja wa serikali akitoa bunduki ndogo kutoka kwenye mshipi aliovalia Pretti kiunoni na kuruka kando.

Dakika chache baadaye, afisa mmoja anaelekeza bunduki yake mgongoni mwa Pretti na kufyatua risasi nne kwa mpigo.

Milio zaidi ya risasi inasikika huku afisa mwingine akionekana akimfyatulia risasi Pretti.

Marais wa zamani Bill Clinton na Barack Obama ni miongoni mwa viongozi wakuu wa chama cha Democrat ambao wamelaani mauaji ya Pretti.