Iran yamnyonga raia wake kwa hofu ni jasusi wa Israel
TEHRAN, IRAN
IRAN Jumatano ilimnyonga mwanaume ambaye alidaiwa kuwa jasusi wa Israel.
Mahakama ya Iran ilitoa taarifa ya kusema mwanaume huyo Hamidreza Sabet Esmaeilipour amenyongwa baada ya kuthibitishwa kuwa alikuwa jasusi wa Israel.
Kutokana na uhasama wa miaka mingi na Israel, Iran imekuwa ikiwanyonga raia wake ambao inashuku wanafanyia Israel ujasusi na kuifichulia shughuli na oparesheni zinazoendelea nchini humo.
“Hamidreza Sabet Esmaeilipour alikamatwa mnamo Aprili 29, 2025 na amenyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kufanyia Israel ujasusi. Uamuzi huu ulitolewa na Mahakama ya Juu kutokana na ushahidi uliowasilishwa na sheria kufuatwa,” ikasema taarifa ya Mahakama ya Juu.
Tangu mwaka jana, raia wa Iran ambao wamekuwa wakinyongwa kwa kufanyia Israel ujasusi imeongezeka sana.
Ongezeko hilo linahusishwa na vita kati ya mataifa hayo mnamo Juni baada ya nchi hizo kuingia vitani.
Mataifa hayo mawili yalipambana vikali kufuatia hatua ya Israel na Amerika kuvamia na kushambulia vituo vya kinuklia.