Wenye matatu watishia kugoma kulalamikia kudhulumiwa na bodaboda
WAMILIKI wa magari ya uchukuzi wa umma wametishia kuanza mgomo kote nchini kuanzia Jumatatu ijayo iwapo serikali itakosa kuchukua hatua kudhibiti dhuluma zinazofanyiwa madereva wa wahudumu wa boda boda.
Wamiliki hao walisema kwamba kuna ongezeko la matukio ambapo wanabodaboda wamekuwa wakichoma moto matatu na magari ya kibinafsi.
Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) kilisema uamuzi huu unafuata matukio yanayohusisha waendeshaji wa pikipiki ambayo yamekuwa hatari kwa abiria na kusababisha usumbufu barabarani.
Chama hicho kimewalaumu wanabod boda kwa kuendesha pikipiki kinyume cha sheria, kuwatishia watumiaji wengine wa barabara na kuingilia kwenye njia za matatu.
Kiongozi wa MOA Albert Karakacha, alisema serikali imekuwa ikishindwa kuwachukulia hatua wahusika licha ya malalamishi ya mara kwa mara kwa idara zinazohusika.
“Tumejaribu mara kwa mara kushughulikia hili na maafisa wa serikali, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa,” alisema Bw Karakacha akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi.
“Iwapo serikali haitachukua hatua, hatutakuwa na chaguo ila kusitisha shughuli zetu ili kulinda wanachama wetu na abiria.”
Aliongeza, “Magari yetu yamechomwa moto; tumezungumza na polisi, tumeandika barua kwa Waziri wa Uchukuzi lakini hakuna kilichofanyika.
“Kuanzia Jumatatu, tutatoa magari yote barabarani hadi pale serikali itakaposikiliza kilio chetu.”