Habari Mseto

Polisi walipia karo msichana aliyepiga guu kilomita 10 kutafuta msaada kituoni mwao

Na GABRIEL KUDAKA, KENROB SIGEI January 29th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

SANDRA Cherono alipoingia katika Kituo cha Polisi cha Kapsabet, Kaunti ya Nandi, Jumanne, maafisa waliokuwapo walidhani alikuwa amefika kuripoti uhalifu au kutoa malalamishi.

Hata hivyo, safari ya Sandra ilikuwa na lengo tofauti kabisa. Alikuwa amesafiri zaidi ya kilomita 10 kuomba msaada wa karo ya shule ili ajiunge na Gredi ya 10.

Cherono, 19 alipata alama 55 katika mtihani wa Gredi 9 na kuitwa Shule ya Ndalat Gaa, Mosop. Akihofia kukosa nafasi hiyo, Sandra aliamua kutafuta msaada katika kituo cha polisi.

Maafisa wa polisi, wakiguswa na ujasiri na azma yake, walichanga fedha kuhakikisha ndoto yake ya kuwa daktari haitoweki.

Wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nandi Samuel Mukuusi, walimnunulia sare, mahitaji binafsi na karo ya mwaka mzima, na hata wakamsafirisha hadi shuleni, umbali wa kilomita 40.