Mkuu wa waasi DRC aapa kuzima muafaka wa kupatia Amerika utajiri wa madini
KINSHASA, DRC
KIONGOZI wa Muungano wa Waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo likiwemo kundi la M23, Corneille Nangaa amepinga muafaka wa madini kati ya Amerika na serikali akisema si wa kikatiba na kuapa kuwa hataruhusu utekelezaji wake.
Nangaa ambaye anaongoza Kundi la Waasi wa AFC, alikuwa anarejelea mkataba uliotiwa saini mnamo Desemba 4, 2025 ambao unaruhusu Amerika kunufaika kwa madini ya DRC.
Kwenye mkataba huo, Amerika nayo itawekeza katika taifa hilo na pia nchi hizo zitashirikiana katika mawanda ya usalama.
Kiongozi huyo anasema mchakato uliofuatwa katika kusaini mkataba huo, haukuwa na uwazi mbali na kuwa na mategu yanayokiuka sheria ya DR Congo.
Kauli ya Nangaa sasa inazidisha utata kuhusu muafaka huo kwa sababu madini mengi yanapatikana mashariki mwa DR Congo, eneo ambalo linadhibitiwa na M23.
“Amerika wamesaini mkataba lakini wanastahili kufahamu kuwa walifanya hivyo na utawala ambao umejaa ufisadi na uko madarakani kiharamu,” akasema Nangaa kwenye mahojiano jijini Goma.
Hata hivyo, afisi ya Rais Felix Tshisekedi, imekanusha kauli ya Nangaa ikisema kuwa kila kitu kilifanywa kwa kufuata sheria za nchi hiyo.
Pia utawala wa Tshisekedi ulisema kuwa stakabadhi yenye maelezo kuhusu muafaka huo itawasilishwa bungeni mnamo Machi ili iidhinishwe.
“Tuna wabunge wengi kwa hivyo tunaamini kwamba itaidhinishwa kisha muafaka huu uanze kufanya kazi au kutekelezwa,” akasema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Uchumi Daniel Mukoko Samba.
Wakati wa mahojiano hayo, Nangaa alikiri kuwa AFC walishirikiana na Rwanda na Uganda kuhusu masuala ya usalama lakini akakanusha vikali kuwa wamewahi kupata msaada wa kijeshi kutoka Kigali.
Rwanda imekuwa ikikanusha kuwa inaunga M23 lakini ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Julai mwaka jana iliihusisha na utoaji zana za kivita na wanajeshi kwa kundi hilo la waasi.
Nangaa pia alishutumu Kinshasha kwa kutatiza juhudi za upatikanaji wa amani akisema mapendekezo yaliyoafikiwa Doha ya kusitisha vita hayajatekelezwa.