Habari

Ruto: Mniache nipange mambo ya 2027 na Oburu

Na RUSHDIE OUDIA January 31st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto Januari 30, 2026 aliwaomba wapigakura kuunga mkono muafaka wa kabla ya uchaguzi kati ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Orange Democratic Movement (ODM) kama msingi wa kuunda serikali ijayo.

Rai hii ya Rais inajiri wakati ODM inakabiliwa na migawanyiko ya ndani kuhusu iwapo ianze mara moja mazungumzo na UDA au isubiri hadi Uchaguzi Mkuu wa 2027 ukikaribia.

Tofauti hizo zimezidi kuchochewa na mvutano kuhusu ni nani anayepaswa kuongoza mazungumzo hayo, huku upande mmoja ukimtaka kiongozi wa chama Dkt Oburu Oginga achukue jukumu hilo, na mwingine ukisisitiza suala hilo liamuliwe kupitia Mkutano Maalum wa Kitaifa wa Wajumbe.

Huku ODM ikitoa ishara mseto kuhusu mwelekeo wake wa kisiasa, Dkt Ruto ameamua kuzipita kamati za vyama na kuelekeza ujumbe wake moja kwa moja kwa wananchi, akiwashawishi wakazi wa Kisumu eneo linalotambuliwa kama ngome ya kisiasa ya familia ya Odinga kuunga mkono maridhiano mapya ya kisiasa kati ya vyama hivyo vikuu nchini.

Akiwa Kisumu jana Rais alisema ushirikiano huo ndio njia pekee ya kukomesha siasa za ukabila, ubaguzi na migawanyiko.

“Leo nawaomba ruhusa, wananchi wa Kisumu, mruhusu UDA na ODM kufanya kazi pamoja na kuunda serikali ijayo. Nipeni ruhusa niketi na Dkt Oburu Oginga tupange serikali mpya itakayokomesha ukabila na uongozi mbaya,” alisema Dkt Ruto.

Alisema hayo akiwa katika eneo la Kondele ambako alipokelewa kwa shangwe na umati mkubwa uliokuwa umemsubiri tangu saa kumi na mbili asubuhi.

Mapema jana, Rais alihudhuria mahafali ya tano ya Chuo Kikuu cha Uzima na kukagua mradi wa nyumba za gharama nafuu unaoendelea Kanyakwar, Kisumu Mashariki.

Wiki iliyopita, katika kikao cha Baraza Simamizi ya Kitaifa la UDA kilichofanyika Ikulu ya Nairobi, Rais alisema muungano anaopanga na ODM kabla ya uchaguzi utamletea ushindi mkubwa wa kura kati ya milioni mbili hadi tatu dhidi ya upinzani mwaka 2027. Alisema makubaliano hayo yatapanua uungwaji mkono wa muungano tawala kitaifa.

Hata hivyo, kumekuwa na hofu kuwa msukumo huo wa muafaka wa kisiasa unafunika ajenda ya vipengele 10 kati ya Rais Ruto na Raila Odinga. Viongozi wa Kisumu walimtaka Rais kuhakikisha suala la fidia kwa waathiriwa wa ghasia za maandamano linashughulikiwa, ikizingatiwa kuwa eneo hilo limekuwa likiathirika zaidi na ghasia.

Rais aliwahakikishia kuwa licha ya mahakama kuzuia kuundwa kwa jopo la fidia, jukumu hilo lipo kwa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR).

“Hata kama walienda mahakamani kuzuia mchakato huu, nitahakikisha kila aliyepoteza maisha au kujeruhiwa akitetea haki zake atafidiwa, kwa sababu ninyi ni mashujaa wa demokrasia nchini Kenya,” alisema.

Rais pia alijigamba kuwa ana uzoefu wa kuunda serikali, akiwabeza wapinzani wake kwa kukosa ajenda, na kusema atawashinda mapema katika uchaguzi ujao.

“Nchini Kenya, kiongozi anachaguliwa kwa misingi ya utendaji wake, si sura, ukabila au maigizo. Kila mmoja aje awaambie wananchi alichowafanyia,” alisema.