Upinzani: Kuna mapungufu kadhaa IEBC
MUUNGANO wa Upinzani umeelezea wasiwasi wake kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ukidai kuwa mapungufu ya kiteknolojia, usalama na uongozi ndani ya tume zinahatarisha uadilifu wa uchaguzi ujao.
Viongozi hao walionya kuwa endapo malalamishi hayatashughulikiwa kwa dhati, nchi inaweza kushuhudia maandamano ya kitaifa.
Baada ya kikao cha faragha na makamishna wa IEBC Jumatano, upinzani ulisema hofu yao inatokana na waliyoshuhudia katika chaguzi ndogo zilizofanyika hivi majuzi na maandalizi ya taasisi hiyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Kulingana nao, IEBC bado inatatizika kurejesha imani ya umma katika mazingira ya kisiasa ya Kenya.
Kiongozi wa Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, alisema upinzani hauridhishwi na mchakato wa ununuzi wa vifaa vya mfumo wa habari za uchaguzi Kenya (KIEMS) na uhusiano wa IEBC na kampuni ya Smartmatic, ambayo imekumbwa na lawama kimataifa. Alionya kuwa maamuzi kuhusu ununuzi wa teknolojia yasiyo wazi yanaweka uhalali wa uchaguzi mashakani.
“Haturidhishwi kabisa na mchakato wa ununuzi wa vifaa vya KIEMS na kampuni ya Smartmatic ambayo imelaumiwa kimataifa,” alisema Bw Musyoka.
Kiongozi wa Democratic Action Party–Kenya, Eugene Wamalwa, alisema teknolojia ya uchaguzi imekuwa chanzo kikuu cha migogoro ya kisiasa nchini kwa miaka mingi. Alisema mifumo ya kampuni ya Smartmatic ilitumika katika nchi jirani kama Uganda, ambako vifaa vilishindwa kufanya kazi, akisema Kenya haipaswi kurudia makosa kama hayo.
“Teknolojia hii hii ilitumika hivi majuzi Uganda. Vifaa vya KIEMS vilikosa kufanya kazi. Hatutaki kuona uchaguzi kama huo Kenya,” alisema Bw Wamalwa, akionya kuwa ukosefu wa uwazi wa kiteknolojia unaweza kuamua matokeo kimyakimya hata kabla ya kura kupigwa.
Vinara hao wa upinzani walisema matatizo ya IEBC hayaishii kwenye teknolojia pekee. Kiongozi wa Democracy for Citizens Party, Rigathi Gachagua, alidai kuwa maafisa wa serikali na makundi yenye ushawishi walivuruga chaguzi ndogo za Novemba mwaka jana, huku vituo vya kupigia kura vikidaiwa kutwaliwa kwa nguvu na wahuni na wanasiasa wa chama tawala.
“Wahuni wao walitwaa vituo vya kupigia kura. Mawaziri walitwaa vituo vya kupigia kura,” alisema Bw Gachagua, akitaja hali hiyo kama kuporomoka kwa mfumo wa usalama wa uchaguzi.
Bw Gachagua alionya kuwa hasira ya umma inaweza kulipuka iwapo hali haitarekebishwa.
Viongozi hao pia walilalamikia madai ya hongo, kukosa kuwajibishwa kwa wanaohusika na ghasia za uchaguzi na kile walichoita utamaduni wa kutochukuliwa hatua.
Aidha, walieleza kutoridhishwa na uongozi wa juu wa IEBC, hasa Afisa Mkuu Mtendaji, Hussein Marjan wakisema udhaifu wa kiutawala umeendelea kudhoofisha Tume.
“Tuliwaambia wazi kuwa hatufurahishwi kabisa na Afisa Mkuu Mtendaji (CEO)” alisema Bw Musyoka.
Naibu Kiongozi wa chama cha Jubilee, Fred Matiang’i, alisema walifungua roho kwa tume.
“Hakuna suala ambalo hatukuligusia—ununuzi, usalama, usimamizi wa chaguzi ndogo, mfumo mzima wa uchaguzi,” alisema Bw Matiang’i,.
Vinara hao pia walielezea wasiwasi kuhusu usajili wa wapiga kura kwa wingi, unalotarajiwa kuanza Machi, wakionya kuwa muda uliopangiwa ni mfupi mno kuongeza idadi ya wapiga kura hasa miongoni mwa vijana.
“Tunaelewa kuwa anafanya kila juhudi kuhakikisha hatuko pamoja, lakini tumeamua hatutaruhusu hilo litokee,” alisema Bw Muturi. “Ikiwa kuna yeyote atakayeamua kwenda upande wake, basi Wakenya watamwadhibu vikali.”
Ili kupunguza mvutano, pande zote zilikubaliana kuunda timu za pamoja za kiufundi kuchunguza masuala ya ununuzi, sheria za uchaguzi na changamoto za kiutendaji. Hata hivyo, upinzani uliendelea kuonya kuwa bila mageuzi ya haraka, maandalizi ya uchaguzi wa 2027 yataendelea kukumbwa na mashaka makubwa.