HabariSiasa

Usitishwe na mbio za Kuria, Ruto aambiwa

February 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ALEX NJERU

WANASIASA wa Mlima Kenya wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, Ijumaa walimpuuza mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, aliposisitiza kuwa atagombea urais 2022.

Akihutubu katika kijiji cha Rubate, eneobunge la Chuka/Igambang’ombe wakati wa mazishi ya Jennifer Cianjagi, mama ya Gavana wa Tharaka Nithi, Muthomi Njuki, Bw Kuria alisema atatangaza chama atakachotumia kugombea urais wakati ukifika.

Alisema baadhi ya watu watashangaa watakapomuona akisindikizwa na magari barabarani kuelekea Ikulu akiwa rais.

“Ninawaomba mniunge mkono niwe rais 2022 lakini nitatangaza chama nitakachotumia kugombea urais wakati ukifika,” alisema Bw Kuria.

Mbunge huyo alisema kwamba ndiye mwanasiasa wa pekee nchini anayeweza kushiriki kampeni na kuwahudumia wapigakura akisema wanaopinga kampeni za mapema wanamuogopa.

Punde tu baada ya kuondoka jukwaani, wanasiasa, wakiongozwa na Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, mwenzake wa Meru Kiraitu Murungi na seneta Mithika Linturi walimpuuza wakisema hatoshi mboga.

Bw Waititu alisema eneo hilo litamuunga Dkt Ruto.

“Hatuchanganyikiwa kuhusu mwelekeo tunaofuata kama watu wa Kiambu. Tunasubiri wakati unaofaa ufike na tutakuunga mkono ( Ruto) kwa sababu ya bidii yako na tunapenda watu wenye bidii,” alisema Bw Waititu.

Alisema ana hakika kwamba Dkt Ruto atakuwa rais 2022.

“Tuna imani nawe na hatutaki kukanganywa na watu wengine,” aliongeza.

Bw Murungi alisema eneo la Meru halitapiga kura kwa watu wasioweza kuwapa maendeleo na kwamba baadhi ya watu ni wapiga kelele.

“Kiongozi anayeunga watu wa Meru ndiye tutakayeunga kwenye uchaguzi wa 2022,” alisema Bw Murungi.

Alimfananisha Bw Kuria na kuku anayepiga kelele baada ya kutaga yai moja ilhali kuna ng’ombe anayekamwa kila siku na kulisha familia kwa maziwa ilhali hapigi kelele.

Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru alisema Kuria sio chaguo la eneo hilo la mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao. Alisema wataendelea kumuunga Dkt Ruto.

Akiongea kwa Kikikuyu, Bi Waiguru alisema “Katika lugha yetu tunasema mundu mugi ndari muhere wa ndeto ( mtu mwerevu hafai kuambiwa mambo mengi). Tunajua kucheza siasa na upande tunaounga. Hakuna anayepaswa kuambiwa na kusema kweli sio upande wa Kuria,” alisema.

Bw Linturi alisema hawezi kumchukulia Bw Kuria kwa umakini na kuongeza kwamba anaamini alikuwa na matatizo.

Wabunge Kimani Icungwa (Kikuyu) na Kareke Mbiuki (Maara) walimweleza Bw Kuria kusalimiana na Dkt Ruto wakisisitiza kuwa Wakenya wameamua kumuunga naibu rais.

Hata hivyo aliposimama kuhutubu, Dkt Ruto aliepuka siasa na kuhakikishia Wakenya kwamba yeye na Rais Uhuru Kenyatta wamejitolea kuwahudumia.

Dkt Ruto aliwahimiza Wakenya kuunga miradi ya maendeleo ya serikali na viongozi wanaopenda maendeleo na sio wale wanaojali maslahi yao ya kibinafsi.