Makala

TAHARIRI: Vijana wakipewa ajira watalipa mikopo ya Helb

February 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

SERIKALI inafaa kutafuta mbinu bora zaidi za kufuatilia watu waliopewa mikopo ya elimu ya juu kupitia bodi ya HELB, badala ya kuwatolea Wakenya vitisho vya kutumia polisi kunasa watu hao.

Tangu mzigo wa kugharimia elimu ulipoanza kugawanywa baina ya serikali na wazazi, ililazimu kuundwa kwa hazina ya kuwalinda wanafunzi maskini wa vyuo vikuu dhidi ya kuacha masomo kwa sababu ya kukosa pesa za kulipa karo.

Ndiposa Bodi ya Kutoa Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) ikaundwa mwaka 1995 kupitia Sheria ya Bunge.

Bodi hiyo ilinuiwa kutoa ufadhili wa kifedha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, hapa nchini na ng’ambo, kupitia mikopo na misaada ya masomo.

Ingawa makusudi yalikuwa mema, changamoto ziliibuka katika utekelezaji na hususan ukusanyaji wa mikopo kutoka kwa walionufaika.

Siku ya Jumatano wakati Waziri wa Elimu Amina Mohamed aliposema HELB itatumia polisi kunasa watu wasiolipa mikopo yao, alifichua kuwa bodi hiyo inadai mikopo ya takriban Sh7.2 bilioni huku baadhi ya watu wakiwa wamegonga miaka 10 bila kuanza kulipa chochote.

Bodi hiyo pia imepoteza fedha kutokana na vifo vya wanafunzi kwa njia moja au nyingine.

Kisa kama kile cha shambulizi la kigaidi dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa mwaka 2015, ambapo wanafunzi 147 waliangamia, kilifanya HELB kupoteza takriban Sh10 milioni.

Vifo vya kawaida vya wanafunzi pia vimedidimiza hazina ya HELB ilhali bodi hiyo bado inahitajika kutimiza jukumu lake la kufadhili masomo ya juu ya wanafunzi – idadi ambayo inazidi kuongezeka huku wanafunzi zaidi wakijiunga na taasisi za elimu ya juu.

Bajeti ya HELB kwa jumla ni Sh11.4 bilioni, nacho kiwango cha mikopo inachodai ni Sh7.2 bilioni.

Ni wazi kwamba bodi hiyo haiwezi kuendesha shughuli zake na vile vile kuwapa wanafunzi wapya mikopo ya elimu ipasavyo.

Changamoto hii ndiyo kiini cha tangazo la Waziri Mohamed. Hata hivyo, suluhu sio kukamata watu ambao hawalipi mikopo, iwe wanafanya kazi ama walimaliza masomo lakini hawajamaliza kulipa mkopo.

Ni kweli kwamba baadhi ya watu wamekuwa katika ajira kwa miaka kadhaa lakini wamekwepa kimakusudi kulipa mikopo yao.

Njia mwafaka zaidi ya serikali kuwanasa ni kutumia mfumo mpya tarajiwa wa Huduma Namba utakaonakili matukio ya kila Mkenya ikiwemo kazi anazoajiriwa.

HELB italazimika kuwa makini kabisa kufuatilia kila mtu anapopata ajira ili wachunguzi wake wafululize hadi kwa mwajiriwa na aanze kukata pesa za mkopo kutoka kwa mshahara wa mhusika.

Serikali pia itahitajika kutatua kwa haraka tatizo la ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana, ambao umefikia asilimia 75 ya vijana, na kuashiria kuwa ni mlima kudai wanafunzi kulipa mikopo ilhali hawawezi kugharamia mahitaji ya kila siku.